Waliopitiwa na mradi wa umeme Singida hadi Namanga kulipwa fidia

October 16, 2018 5:53 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mradi huo wa kusafirisha umeme utaunganisha nchi za Tanzania na Kenya ili kuongeza fursa za upatikanaji wa umeme katika nchi hizo.
  • Vijiji 14 vilivyopitiwa na mradi vitapata umeme ambapo vijiji saba ni vya mkoa wa Singida, viwili kutoka Manyara na vitano ni vya mkoa wa Arusha.
  • Kukamilika kwa mradi huo  kutaiwezesha Serikali kuuza umeme katika nchi za Afrika Mashariki.
  • Utafungua fursa za ajira kwa vijana mpaka utakapokamilika Februari 2020.

Dar es Salaam. Serikali imeanza kulipa fidia kwa wananchi 4,000 waliopisha mradi wa kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga mkoani Arusha.

Mradi huo wa kusafirisha umeme utaunganisha nchi za Tanzania na Kenya ili kuongeza fursa za upatikanaji wa umeme katika nchi hizo.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa kazi za awali za utekelezaji wa mradi huo zilikwishaanza na kinachosubiriwa sasa ni kukamisha zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi husika ili wakandarasi waanze rasmi kazi ya ujenzi.

Mgalu ameweka wazi kuwa, katika utekelezaji wa mradi huo, vijiji 14 vilivyopitiwa na mradi vitapata umeme ambapo vijiji saba ni vya mkoa wa Singida, viwili kutoka Manyara na vitano ni vya mkoa wa Arusha.

Mradi huo utawezesha ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme mjini Arusha na kupanua kituo cha kupoza umeme mkoani Singida.

Kukamilika kwa mradi huo  kutaiwezesha Serikali kuuza umeme katika nchi za Afrika Mashariki kupitia ushirikiano wa pamoja katika Sekta ya Nishati ujulikanao kama East African Power Pool, (EAPP) unaoshirikisha nchi za Uganda, Ethiopia, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Kenya.


Zinazohusiana:


Mkuu wa Wilaya na Hanang, John Mkirikiti amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo uzingatie na kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wenye nguvu walio katika maeneo yanayopitiwa na mradi.

Ameahidi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo hususan kuimarisha ulinzi na usalama, na kuwataka vijana watakaopata fursa ya kufanya kazi katika mradi kuwa waaminifu na walinzi wa miundombinu hiyo ya umeme.

Naye Meneja Msimamizi Mkuu wa Utekelezaji wa Mradi huo, kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Mhandisi Oscar Kanyama amesema kuwa upande wa Tanzania mradi huo utajengwa kwa urefu wa kilometa 414 na kwa upande wa Kenya utajengwa kwa urefu wa kilometa 96 kutoka kituo cha kupoza umeme Isinya hadi Namanga.

Mhandisi Kanyama amesema mapema Novemba, kazi za kuchimba mashimo pamoja mitaro kwa ajili ya kujenga misingi ya mradi huo itaanza.

Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania iliyotoa Dola za Marekani milioni 44, Wadau wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iliyotoa Dola za Marekani milioni 258 na Shirika la Mandeleo la Japani ( JICA) lililotoa Dola za Marekani milioni 89, mradi huo unatarajia kukamilika Februari 2020.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) alipotembelea eneo la kuhifadhia vifaa vya mradi huo katika kijiji cha Nangwa wilayani Hanang mkoani Manyara. Picha| Wizara ya Nishati.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW