Vuta nikuvute mradi wa Mchuchuma, Liganga bungeni

June 20, 2019 9:16 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wabunge wa mkoa wa Njombe wambana Waziri kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe.
  • Naibu Waziri Manyanya asema wanakwamishwa na mwekezaji anayetaka vipaumbele vipya vya uwekezaji. 
  • Serikali yasema muda wa mwaka mmoja uliobaki haiwezi kuutekeleza kikamilifu. 

Dar es Salaam. Unaweza kusema, leo katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni kilitawaliwa na mjadala wa mradi wa Mchuchuma na Liganga baada ya Wabunge kumbana kwa maswali Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya juu ya kuchelewa kwa utekelezaji wa  mradi huo. 

Mradi huo ni wa kimkakati wa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021 kwa ajili ya uchimbaji na uchakataji wa madini ya chuma na makaa ya mawe yanayopatikana wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Mjadala huo ulihusisha wabunge wa mkoa wa Njombe leo (Juni 20, 2019) ambapo Mbunge wa Viti Maalum, Lucia Mlowe alianza kuuliza swali kuwa Serikali itaanza lini kutekeleza mradi huo kwa sababu imekuwa ikitoa ahadi kwa  wananchi ambao wana shauku ya kuona unaanza kufanya kazi. 

Akijibu swali hilo, Mhandisi Manyanya amesema sababu ya kuchelewa kwa mradi huo ni kuibuka kwa changamoto ya kutoelewana kati ya mwekazaji wa mradi huyo kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd ya China kuhusu vivutio vya uwekezaji ambavyo anataka viwekwe kwenye mradi.

“Changamoto kubwa iliyojitokeza ni majadiliano kati ya mwekezaji na Serikali kuhusu vivutio vya uwekezaji kuchukua muda mrefu kutokana na mwekezaji kutaka vivutio vya ziada ambavyo haviko kisheria.

“Tutaendelea kujadiliana naye ili aone uwezekano wa kurekebisha vivutio anavyovitaka na kama atashindwa tutamtafuta mwekezaji mwingine mwenye uwezo lakini hiyo siyo kazi ya siku moja,” amesema Naibu Waziri huyo.  


Soma zaidi: 


Amesema kwa sasa, mradi huo uko katika hatua za awali ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu na usanifu; ujenzi wa barabara hadi eneo la mradi na kufanya tathmini ya mradi wote na maeneo wananchi watakayopisha mradi. 

“Hivyo, Serikali inaangalia njia bora ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa tija ili kuleta manufaa mapana kwa wananchi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla,” amesisitiza Mhandisi Manyanya. 

Baada ya majibu hayo akasimama Mbunge wa Ludewa, Deo Galawa na kutoa hoja ya kuwa mradi huo ni wa muda mrefu lakini haupewi kipaumbele ukilinganisha na miradi mingine ambayo inatekelezwa kwa kasi licha ya kuanza hivi karibuni. 

Akitolewa ufafanuzi swali hilo, Manyanya amesema bado wanautambua mradi huo lakini kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo  ujenzi wa bwawa la kuzalishaji umeme katika mto Rufiji mkoani Pwani na ujenzi reli ya kisasa ya SGR. 

Amebainisha kuwa kinachofanyika sasa ni kuwalipa fidia wananchi waliondolewa kupisha mradi huo ili Serikali ianze kutekeleza mradi huo pale itakapoona inafaa. 

Mradi huo ni wa kimkakati wa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021 kwa ajili ya uchimbaji na uchakataji wa madini ya chuma na makaa ya mawe yanayopatikana wilayani Ludewa mkoani Njombe.Picha|Mtandao.

Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), watu takriban 1,145 watalipwa fidia kupisha mradi wa kuzalisha chuma wa Liganga mwaka huu. 

Kama hiyo haitoshi, akasimama Mbunge mwingine  wa Viti Maalum mkoa wa Njombe, Neema Mgaya na kusema mradi huo ni wa mkakati na ulipaswa utekelezwe kati ya mwaka 2015/2016 na 2020/2021 na umebaki mwaka mmoja, Serikali itaweza kuukamilisha katika kipindi hicho kifupi kilichobaki?

Katika kujibu hoja hiyo Manyanya amesema “kwa mwaka huu mmoja mimi naamini hatutaweza kukamilisha lakini hatua hizo zimeanza na kwa mradi mkubwa kama huu huwezi kuutekeleza kwa mwaka mmoja.”

“Lakini napenda kusisitiza lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha tunautekeleza mradi huu kwa tija na mali iliyopo pale inawahudumiwa Watanzania kwanza na mwekezaji naye afaidike,” ameongeza Manyanya ambaye pia ni Mbunge kutoka Nyasa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW