Sifa za mtu anayetakiwa kusimamia mirathi
- Anatakiwa kuteuliwa na marehemu wakati wa uhai au kikao cha ukoo.
- Anatakiwa kutambuliwa na mahakama.
Dar es Salaam. Mirathi ni taratibu mbalimbali za kisheria zinazoongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi na hatimaye ugawaji wa mali na hata kumaliza madeni ya marehemu pamoja na mazishi.
Baada ya kufahamu maana ya mirathi, tuangazie mtu anayepaswa kusimamia mirathi kwenye familia.
Msimamizi wa mirathi ni nani?
Ni mtu ambaye anateuliwa kusimamia mali ambazo zimeachwa na marehemu. Ni mtu ambaye anavaa viatu vya marehemu na kushughulika na mali za marehemu na mambo yote yaliyokua yanamuhusu marehemu wakati wa uhai wake. Na anapaswa kufanya vile ambavyo marehemu angefanya wakati wa uhai wake.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mirathi ya mwaka 2002 imeainisha kinaga ubaga majukumu na kazi za msimamizi wa mirathi.
Msimamizi wa mirathi anateuliwa na Nani?
Msimmaizi wa mirathi anaweza kuteuliwa na marehemu wakati wa uhai wake endapo marehemu atakua ameacha wosia. Ikiwa marehemu hajaacha wosia basi kikao cha ukoo kitaketi na kuteua msimamizi wa mirathi.
Msimamizi wa mirathi analazimika kwenda mahakamani ili kupata barua rasmi ambayo itamtambulisha kama msimamizi wa mirathi kama ilivyoanishwa na sehemu ya tano ya sheria ya Sheria ya Usimamizi wa Mirathi sura ya 352 R.E ya 2002.
MAJUKUMU YA MSIMAMIZI WA MIRATHI
- Kukusanya mali za marehemu
Jukumu la kwanza la msingi la msimamizi wa mirathi ni kuweza kukusanya na kutambua mali zote za marehemu. Anatakiwa kuzijua na kuziainisha vizuri.
Soma zaidi:
- Mahakama Tanzania ni mwendo wa dijitali utoaji huduma
- Apps za elimu zinazoweza kuwaelimisha watoto wadogo kabla ya kwenda shule
2. Kuwa mwakilishi wa kisheria wa marehemu
Msimamizi wa mirathi anakua anavaa viatu vya marehemu na anapaswa kusimama kwenye majukumu ya marehemu yote. Ikiwa marehemu anamdai mtu ama amefungua kesi au amefunguliwa kesi basi msimamizi wa mirathi ndiyo anapaswa kufika mahakamani na kujibu madai yote yaliyowasilishwa dhidi au na marehemu.
Dhana hii inatumika kwenye mashauri ya madai tu na haitumiki kwenye jinai. Kifungu cha 99 cha sheria Sheria ya Usimamizi wa Mirathi sura ya 352 R.E ya 2002 kimeanisha haya kwa undani.
- Kukusanya na kulipa madeni ya marehemu
Ni wajibu wake kisheria kukusanya na kulipa madeni yote ambayo marehemu alikua anadaiwa kipindi cha uhai wake. Kisheria ana wajibu wa kufungua kesi ili kukusanya madeni yote ambayo marehemu alikua anadai. Kifungu cha 100 cha Sheria ya Usimamizi wa Mirathi sura ya 352 R.E ya 2002 kimempa nguvu hiyo.
- Kuuza au kukodisha mali za marehemu
Msimamizi wa mirathi ana haki ya kuuza mali za marehemu au kukodisha kwa namna yoyote ile ambayo anaona inafaaa na iko sahihi kisheria. Kifungu cha 101 cha Sheria ya Usimamizi wa Mirathi sura ya 352 R.E ya 2002 kinaeleza kuwa msimamzi wa mirathi anaweza kuuza mali za marehemu pasipo kupewa ridhaa na wanufaikaji wa mali za marehemu isipokua tu uuzaji wake umefanywa kisheria na umekidhi matakwa ya kisheria na kwa faida ya wanaufaikaji na sio faida yake binafsi.
- Kugawanya mali za marehemu
Moja ya jukumu lake zito ni kugawanya mali zote za marehemu kwa wanufaikaji bila upendeleo wa aina yoyote ile. Anatakiwa kuhakikisha kuwa wanufaikaji halali wote wanapata mgao kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria zinazosimamia mirathi husika . Msimamizi anatakiwa kuhakikisha hakia za watu wote zinazingatiwa wakati wa ugawaji wa mali za marehemu kuepusha malalamiko yasiyo na msingi.
- Kulipa gharama za mazishi
Shughuli za mazishi ni gharama kwa sababu kifo ni jambo la ghafla basi madeni mengi yanaibuka kutokana na kusimamia shughuli za mazishi, msimamizi wa mirathi anatakiwa kuhakiakisha gharama zote hizi zinalipwa.
- Kufunga mirathi
Baada ya kugawanya mali zote kwa wanufaikaji wa mirathi ya marehemu, anapaswa kupeleka taarifa mahakamani. Ripoti hii inatakiwa kuonyesha jinsi zoezi zima lilivyoendeshwa na ukamilifu wake. Msimamizi anatakiwa kupeleka ripoti mahakamani ndani ya miezi 6 tangu kupewa barua ya usimamizi wa mirathi ya marehemu.
Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,
Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini
Twiter: @Hamzaalbhanj
Simu 0717521700
Latest