Serikali yafunguka daktari aliyezushiwa kupata madhara ya chanjo ya Uviko-19
Mdahalo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima (anayezungumza) ulifanyika Agosti 12, 2021 katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ulikuwa na wawasilisha mada 20 ambapo Dk Bulugu alikuwa mmoja wa wawasilishaji mada pia. Picha| Wizara ya Afya.
- Ni Dk Sospeter Bulugu, mmoja wa wawasilisha mada katika mdahalo wa wanasayansi jijini Dar es Salaam.
- Alipata changamoto za kiafya na kushindwa kuendelea kutoa mada yake.
- Wazushi wamehusisha tukio hilo na madhara ya chanjo ya Uviko-19, Serikali yakanusha.
Dar es Salaam. Serikali imesema siyo kweli madhara ya chanjo ya uviko-19 ndiyo yaliyomfanya Dk Sospeter Bulugu kushindwa kuendelea kuwasilisha mada yake jana katika mdahalo wanasayansi kuhusu Uviko-19 bali ni changamoto za kiafya za kawaida ambazo zilisababishwa na kushuka kwa damu mwilini.
Mdahalo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ulifanyika Agosti 12, 2021 katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ulikuwa na wawasilisha mada 20 ambapo Dk Bulugu alikuwa mmoja wa wawasilishaji mada pia.
Wakati Dk Bulugu ambaye ni Kamishna wa Afya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso) akiongea mada yake alipata hali ya kizunguzungu na hivyo wataalam kulazimika kumpatia huduma ya kwanza.
“Uchunguzi ulionyesha hali hiyo ilitokana na kushuka kwa sukari kwenye damu ambayo kitaalamu inajulikana kama hypoglycemia,” amesema Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe.
Dk Sichalwe amesema hali iliyompata Dk Bulugu huenda pia ilichangiwa na ukweli kuwa mdahalo huo ulifanyika tangu saa 3 hadi 8:30 bila mapumziko ya chai.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya watu waliokuwepo ukumbini hapo walichukua video na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii na kudai kuwa kilichomkuta Dk Bulugu ni matokeo ya kuchanjwa chanjo ya Corona.
Kwenye video hiyo, Dk Gwajima amesikika akihoji iwapo Dk Bulugu alikuwa amepata chanjo na ilipothibitika hakupata ya Uviko-19 sauti ya Waziri wa Afya ilisikika tena ikisema, basi amepatwa na kushuka kwa sukari hasa ukizingatia tangu kuanza kwa mkutano huu hakukuwa na mapumziko ya chai.
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI:-
UFAFANUZI KUHUSU DKT. SOSPETER BULUGU KUSHINDWA KUSOMA HOTUBA YAKE WAKATI WA MDAHALO WA KISAYANSI KUHUSU UVIKO 19 KATIKA UKUMBI WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE, JIJINI DAR ES SALAAM
TAREHE 12/08/2021. pic.twitter.com/zEqLvyQZdk— Wizara ya Afya Tanzania (@wizara_afyatz) August 13, 2021
Madai hayo hayana msingi wowote
Dk Sichalwe katika taarifa yake iliyotolewa leo Agosti 13, 2021 kuhusu madai hayo amesema Dk Bulugu hakuwai kupata chanjo ya Uviko-19 na hivyo uzushi unaonezwa na watu mitandaoni siyo wa kweli.
“Wapo waliochukua (video) na kuzisambaza, matokeo yake zimetumika kupotosha vikihusisha tukio hilo la madhara ya chanjo, jambo ambalo siyo kweli,” amesema Mganga mkuu huyo wa Serikali.
Pia amebainisha kuwa katika ukumbi huo wa mikutano hakukuwa na zoezi la uchanjaji chanjo na Dk Bulugu alikuwa amekwenda kupata elimu kuhusu chanjo hiyo.
“Aidha, wapuuze madai kuwa Waziri wa Afya, alitaka kuficha jambo kuhusu madhara ya chanjo kwani kuvitaka vyombo vya habari visichukue tukio (la Dk Bulugu), Waziri wa Afya alikuwa anatekeleza majukumu yake ya maadili ya kitaaluma pale panapokuwa na mteja anayepokea huduma za afya ambaye hajaridhia kwa hiari yake kwamba huduma hiyo iwe wazi,” amesisitiza Dk Sichwalwe.
Wananchi wametakiwa kupuuza taarifa hizo kwani zinalenga kuvuruga zoezi la utoaji chanjo katika maeneo mbalimbali nchini.
Latest