Imewezekana: Simulizi ya wanawake ‘waliopindua meza’ Dar

September 8, 2021 6:33 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wameachana na kukaa nyumbani na kuanza kuchapa kazi sokoni.
  • Wameongeza kipato cha familia na kuacha utegemezi kwa wanaume.
  • Bado wanakumbwa na changamoto ya uongozi, tozo na umaarufu wa soko.

Dar es Salaam. Endapo muda utarudishwa nyuma kwa miaka 20 iliyopita, bila shaka ingekuwa kawaida kumkuta mwanamke akiwa amekaa nyumbani akisubiri kila hitaji lake litimizwe na mume wake. 

Katika kipindi hicho kutokana na mifumo ya kijamii, ni wachache walioona kujishughulisha katika biashara kama fursa ya kuinuka kiuchumi.

Hata hivyo, mambo yamebadilika. Wanawake wamekuwa vinara katika kila fursa ya kuingiza kipato inayojitokeza mbele yao. Utawakuta barabarani, sokoni na hata ofisini wakijishughulisha kutafuta kesho yao.

Katika Soko la Kinyerezi lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam, wanawake wanasema soko hilo kwao ni “pepo ya kibiashara” kwa sababu imewapunguzia utegemezi wa kiuchumi na kuwapa hamasa ya kutumia uwezo wao kujipatia kipato kwa kuuza bidhaa za nyumbani.

“Mambo yamebadilika kusubiri uletewe kila kitu ni zama za zamani sasa hivi sharti kusaidiana katika familia,” anasema Stella Mwandri anayeuza mboga mboga katika soko hilo.

Stella, anayeshirikiana na mdogo wake kufanya biashara hiyo, anasema fedha anazopata zimekuwa msaada kwa mume wake hasa anapopata changamoto ya kutokukidhi mahitaji yote ya familia. 

Mama huyo, aliyeanza kufanya biashara katika soko hilo mwanzoni mwa mwaka huu, anasema wanawake ambao bado wapo nyumbani, waungane na wenzao kuamka na kuunga juhudi za mapambano ya kujikomboa kukataa “ugoli kipa” (kusubiri kufanyiwa kila kitu na wanaume).

Stella Mwandri amesema kuuza bidhaa kwenye sehemu rasmi kumempatia wateja wengi zaidi. Picha| Gift Mijoe.

Unaweza kuuza popote

“Siyo lazima uwe sokoni tu, hata hapo  nyumbani unaweza anzisha genge lako  na biashara ukafanya,” anasema Stella huku akionyesha tabasamu usoni.

Stella na wanawake wengine wa Ilala walipata nguvu ya kufanya shughuli za kiuchumi hasa sokoni baada ya kujengewa uwezo na shirika lisilokuwa la kiserikali la Equality for Growth (EFG).

EFG na mshirika wake Shirika la Twaweza ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na uongozi wa soko la Kinyerezi kwa zaidi ya miaka mitano sasa, wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake kuzifahamu haki zao na kuzipambania, kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

“Wadau wametufundisha umoja ambapo imefikia hadi sisi wana mama tunajikwamua wenyewe, tunajinyanyua, tuna Vikoba, tuna michezo, tuna mikopo ambayo tumechukua,” amesema Bertha Mtono, mfanyabiashara katika soko la Kinyerezi. 

Hali ilivyokuwa awali

Haikuwa rahisi kwa wanawake kuendesha biashara katika soko hilo hapo awali lakini elimu ya uraghabishi iliyotolewa imesaidia wanawake kupata heshima na kushirikishwa katika maendeleo ya soko hilo.

Mwenyekiti wa mpito wa soko hilo, Philomena Kilegu anasema kabla ya uraghabishi, wanawake walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawaji wa maeneo ya kufanyia biashara na yaliyokuwa yakipatikana yalikuwa yakihusishwa na vitendo vya rushwa.

Pia, wanadai kuwa hapakuwa na tozo zinazolingana kwa watu wote wanaopata maeneo hayo na wanawake walikuwa wakipangiwa kiasi kikubwa ili washindwe kulipia na wasipate sehemu za kuendesha biashara zao.

“Hakukuwa na kiwango, walikuwa wanakuangalia wanakwambia ukitaka tukupe eneo, tupe Sh100,000. Sasa hivi tupo apa ukitaka eneo lipia umeme, lipia ulinzi na mifuko ya dharura,” anasema Kilegu ambaye alitaja tozo za sokoni kuwa ni Sh500 kwa wenye mabanda na Sh300 kwa wenye meza.

Kwa sasa Soko la Kinyerezi limetoa fursa kwa watu zaidi ya 50 kufanya biashara huku wanawake wakiwa ni wengi kwa asilimia 70 ikilinganishwa na wanaume.

Mfanyabiashara mwingine katika soko hilo Yunia Elias, limemsaidia kukutana na watu wapya ambao wamekuwa sehemu ya furaha yake na wanamsaidia kujikwamua na changamoto za kimaisha ikiwemo za familia.

Baadhi ya wadau waliofanya kazi na wanawake hao wanaeleza kuwa awali walikuwa wananyanyaswa na kutengwa katika ugawaji wa maeneo ya kufanyiwa biashara huku wakishawishiwa kutoa rushwa ikiwemo ya ngono.

“Kama mmeona sasa hivi wanawake wapo wenyeviti, wanaoshikilia nafasi za juu za uongozi,” amesema Afisa Mradi wa Equality for Growth (EfG), Susan Sitta akiongelea namna wanawake walivyochangamkia fursa zakufanya biashara katika masoko mbalimbali. 

                       

Tamu lakini ina uchungu

Mbali na kuwa soko hilo kuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 500 kwa wakati mmoja, kwa sasa lina watu chini ya 60 huku wengi wakiondoka kwa kukosa wateja wa uhakika. 

Hata hivyo, wafanyabiashara wanaamini siku zijazo soko hilo litakuwa kubwa na kuvutia watu wengi kama ilivyo kwa masoko mengine ambayo ni maarufu kama Buguruni na Kariakoo.

Changamoto nyingine ya kufanyiwa kazi, wafanyabiashara wanasema ni ushuru ambao hauendani na faida na gharama za biashara wanazotumia kila siku.

Kwa wiki wanatozwa Sh3,000 na pesa hiyo ni ya halmashauri pekee huku wakitakiwa kulipia fedha za ulinzi na umeme ambazo zinajitegemea.

“Siku nzima kaka umeona huko mabanda yamefungwa hamna watu. Wote wameondoka kwa sababu biashara hamna alafu unakuja kuambiwa ulipe pesa ya tozo inatoka wapi na haujauza chochote,” anasema Zubeda Saidi ambaye anauza nywele bandia na vifaa vya urembo. 

Anasema mara nyingi biashara ipo siku ya mnada unaofanyika siku ya Jamatatu ambapo watu huenda sokoni na kununua bidhaa za jumla na kisha kupotea kabisa eneo la soko hilo kwa wiki nzima na baadhi kurudi sokoni kuanzia alhamisi.

Kukosekana kwa wateja, kwa mujibu wa Kilegu, kunatokana na wafanyabiashara kupanga bidhaa zao kandokando ya barabara ya Kinyerezi na kituo cha Kinyerezi Mwisho hivyo kuvutia watu wengi zaidi kuliko soko lenyewe.

Soko la Kinyerezi ambalo kwa sasa lina wafanyabiashara wa chache linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Picha| Gift Mijoe.

Nini kinafuata? 

Ikiwa changamoto kubwa ni tozo, barabara mbovu na uongozi kutiliwa mashaka sokoni hapo, Serikali ya mtaa wa Kinyerezi inayosimamia soko hilo inasema inazitambua changamoto zote na inazifanyia kazi ikiwemo kusimamia upatikanaji wa viongozi.

Ili kufikia viwango bora, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu anasema kwa sasa wanaendelea kuboresha miundombinu ya soko hilo ikiwemo ujenzi wa choo na kisima cha maji ili lizinduliwe rasmi.

Pamoja na kuwa wanawake wanajituma katika biashara, iwapo changamoto hizo hazitatuliwa katika soko hilo huenda zikachangia kuwakatisha tamaa na kuyumbisha mitaji yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW