Tanzania inavyoweza kutokomeza umaskini wa watoto

March 18, 2022 8:44 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

                   


  • Ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika masuala ya watoto.
  • Wazazi na jamii kutambua wajibu wao kwa watoto.

Dar es Salaam. Wataalamu wa masula ya watoto wanaeleza kuwa sababu ya kuwepo kwa umaskini wa mtoto ni pamoja na kaya kuwa na kipato cha chini na familia kuishi katika mazingira hatarishi hasa katika maeneo yasiyo na huduma za kijamii za uhakika ikiwemo maji na elimu.

Afisa Mwandamizi wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Getrude Gyabene anaeleza kuwa hata kuvunjika kwa ndoa, na familia kuwa na watoto wengi hufanya familia kushindwa kumudu gharama za kimaisha na kusababisha watoto kuishi katika hali ya umaskini.

“Watoto wengi wanatumbukia kwenye hilo wimbi la umaskini kutokana na ndoa kuvunjika, wazazi wao kushindwana, unakuta hakuna anayemjali mtoto,” anasema Gyabene.

Umaskini una athari mbalimbali kwa ustawi wa maisha ya watoto  ikiwemo kuwakosesha haki zao za msingi ikiwemo haki ya kupata kupata elimu bora, kucheza na kuishi katika mazingira salama. 

Licha ya kuwa, Tanzania inatoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, bado zipo kaya ambazo zinashindwa kumudu gharama nyingine za kielimu na hivyo kuwafanya watoto wao kuendelea kuishi katika umaskini.

Mtaalamu wa masuala ya haki za watoto na utawala kutoka katika shirika la Save The Children, Wilbert Muchunguzi anaeleza kuwa watoto wanaoishi katika hali ya umaskini hushindwa kukidhi mahitaji yao shuleni na hivyo kuwekwa katika hatari ya kufeli masomo darasani. 

“Serikali imeshaweka hela za kuwasomesha hawa watoto , lakini mzazi ana wajibu wa kununua vitabu, uniform (sare za shule), nauli, chakula, kama familia haina uwezo wa kutoa hivyo vitu kwa mtoto, itamfanya mtoto asiende shule,” anasema Muchunguzi.

Muchunguzi anaongeza kuwa watoto hao pia hukosa lishe bora na kusababisha kupata magonjwa kama utapiamlo na udumavu ambayo yanaathari kubwa hata wanapokuwa watu wazima na wakati mwingine kupoteza maisha.

“Lishe ni kitu cha muhimu sana, tena lishe bora, mtoto akiikosa utakuta anapata utapiamlo, udumavu, na wengine hadi wanafariki,” anasema Muchunguzi.


Zinazohusiana:


Umaskini wa mtoto hauwaathiri watoto pekee bali hata Taifa kwa sababu  wao ni nguvukazi ya baadaye inayotegemewa katika uzalishaji na kukuza uchumi wa nchi.

Watalaamu wanaeleza kuwa umaskini wa mtoto unaweza kutokomezwa nchini endapo  wazazi na jamii watatambua wajibu walionao katika kumlea na kumkuza mtoto katika mazingira salama na rafiki.

“Wazazi wanapaswa kutambua kwamba nikiwa na mtoto majukumu yangu ni haya, natakiwa nihakikishe kuwa anakula, anavaa, anapata huduma za afya, anakua katika sehemu salama na anenda shule,”  anaeleza Gyabene.

Kwa watoto ambao hawana wazazi, au wale wanaokosa huduma za msingi kutokana na kaya kuwa maskini, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanapaswa kuwasaidia watoto hao ili wasiachwe nyuma. 

“ Kuna mifumo imewekwa na Serikali ya kusaidia familia maskini mfano TASAF, lakini Serikali iendelee kuweka mifumo ya kusaidia kwa sababu kuna familia mbazo mzazi anapambana lakini anakosa pesa,” anasisitiza Gyabene.

Sambamba na hilo ni kuongeza uwekezaji katika masuala ya watoto ili kuondokana kabisa na umaskini wa mtoto Tanzania.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira bora na salama, huku akisisitiza kuongeza elimu ya malezi kwa watoto na kuwalinda dhidi ya mambo yasiyofaa kwenye jamii.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW