Bajeti 2022-23 kutoa unafuu wa maisha, kufufua uchumi Tanzania
- Itasaidia kuleta unafuu kwa wananchi
- Uchumi kufufuliwa baada ya kuathiriwa na Uviko-19 na vita ya Urusi na Ukraine
- Mapambano ya vitendo vya rushwa kutiliwa mkazo.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema mapendekezo yaliyopo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2022/23 yamelenga kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi pamoja na kufufua uchumi baada ya kuathiriwa na Uviko-19 na madhara ya vita ya Urusi na Ukraine.
Katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2022/23 Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema Uviko-19 na vita inayoendelea Ulaya Mashariki imeathiri mwenendo wa uchumi na sasa Serikali inaangazia namna ya kuwapatia Watanzania ahueni.
“Nchi ya Urusi ni ya pili katika uzalishaji wa gesi asilia na bidhaa za mafuta ya petroli duniani. Kadhalika, nchi ya Ukraine ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta ya alizeti kwa wingi duniani. Kufuatia madhara haya ya vita, ni dhahiri kuwa uchumi na gharama za maisha duniani hazitabaki zilivyokuwa awali,” Dk Nchemba amesema.
Dk Mwigulu amesema bungeni jijini Dodoma leo (Juni 14, 2022) kuwa bajeti hiyo itatilia mkazo sera za mapato, sera za matumizi, kujali ufanisi (Value for Money), mapambano ya vitendo vya rushwa na kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ili kutengeneza ajira kwa vijana.
Dk Nchemba ameongeza kuwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani, nchi za Urusi na Ukraine ni kati ya nchi zenye uzalishaji na uuzaji mkubwa wa mazao mbalimbali ikiwemo ngano, mafuta ya kula na shayiri.
Latest
