Majaliwa: Zingatieni uadilifu ujenzi wa mji wa Serikali

Baadhi ya majengo yaliyopo kwenye mji wa serikali Mtumba Dodoma|Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Ni viongozi waliopewa dhamana ya ujenzi wa mji wa Serikali Dodoma.
- Mji huo kukamilika Oktoba 2023.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali kuzingatia uadilifu katika matumizi ya fedha ili waweze kukamilisha ujenzi kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Septemba 5, 2022 alipokuwa akizungumza baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ujenzi wa Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma, ambapo amewashukuru na kuwapongeza wakandarasi wanaojenga mji huo.
“Lazima tujivunie maono ya viongozi na kazi nzuri wanayoifanya pamoja na kazi nzuri za wataalamu wetu.” amesema Majaliwa.
Serikali ilitangaza rasmi kuhamia Dodoma mwaka 2016 na utekelezaji wake kuanza rasmi mwaka 2019 kwenye kipindi cha uongozi wa Rais Hayati John Magufuli.
Tangu kipindi hicho viongozi mbalimbali wa Serikali wamekuwa wakihamia kwenye mji hupo mpya huku ujenzi wake ukiendelea ambapo unakadiriwa kukamilika ifikapo Octoba 2023.
soma zaidi
“Fedha za kutekeleza haya zipo na ninawahakikishia kila kitu kitakamilika, dhamira ya Rais Mheshimiwa Samia ni kufanya makao makuu kuwa bora zaidi,” amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa akiwa jijini hapo amekagua majengo ya wizara tano ikiwemo jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, na Utaratibu, jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na jengo la Ofisi ya Rais Tamisemi.
Majengo mengine yaliyokaguliwa ni pamoja na jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii, jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na ujenzi wa jengo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mradi huo wa ujenzi wa nyumba za Serikali kwa awamu ya pili unakadiriwa kutumia Sh675 bilioni mpaka kukamilika kwake ambapo utakuwa na majengo majengo 25 ya wizara pamoja na majengo mawili ya taasisi za umma.
Vijana zingatieni maelekezo
Majaliwa amewasisitiza vijana wanaofanya kazi katika mradi huo waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na maelekezo wanayopewa na viongozi wao ili wawe na uwezo wa kujenga na kusimamia kazi zao.
“Mradi huo unajengwa na wakandarasi tisa wakiwemo wa Serikali na binafsi, umetoa ajira 2,149,” anasema Mratibu wa Mradi wa Ujenzi huo Meshack Bandawe.
Latest