Pendo Boshe: ‘Kichwa’ cha Vodacom chenye mafunzo lukuki kwa watoto wakike Tanzania
- Ni moja ya Wahandisi mahiri wanawake katika Sekta ya Mawasiliano Tanzania.
- Huanza siku yake Saa 10.30 alfajiri kwa sala, kuandaa chai na kuwapeleka watoto shule.
- Anaamini kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kuchochea uvumbuzi na kuchangia ukuaji wa taasisi mbalimbali.
Kulikuwa na dhana ya muda mrefu kuwa kazi za uhandisi ni za wanaume. Hata hivyo, zama zimebadilika. Hivi sasa wanawake nao wanasomea kozi hiyo huku wakifanya kazi katika uwezo mkubwa.
Leo (Aprili 26 2018) ulimwengu unaadhimisha siku ya kuhamasisha wasichana kujihusisha na kunuifaka na Tehama (Girls in ICT). Siku hiyo huratibiwa na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU).
Katika kuadhimisha siku hiyo tunaangazia kazi ya Pendo Boshe, Mhandisi wa mtandao wa kampuni ya huduma za simu ya Vodacom ambaye ni moja ya wanawake wachache ambao historia yao inaweza kuwapa hamasa watoto wa kike kupenda zaidi masomo ya Uhandisi na Tehama.
Katika mahojiano yaliyofanyika wakati wa kuelekea Siku ya kuhamasisha watoto wakike na Wanawake vijana kusoma Tehama, Pendo anaeleza vikwazo wanavyokumbana navyo wanawake kwenye taaluma hiyo, namna ya kujikwamua na jinsi gani waajiri wanaweza kuwasaidia kuvishinda. Pia, anaangazia uzoefu wake katika kazi ambayo watendaji wake wengi ni wanaume.

Upendo Boshe akiwa ofisini kwake hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Pendo ni nani?
Mimi ni mhandisi kitaaluma, mama na mke. Nilimaliza Shahada ya Sayansi ya Uhandisi Umeme mwaka 2002 na baadaye mwaka 2010 nilitunukiwa Shahada ya Uzamili ya uhandisi ya Usimamizi wa Miradi. Nilijiunga Vodacom mwaka 2002 kama Mthibiti wa Mtandao na kazi kuu ilikuwa ni kufuatilia, kutathmini utendaji na kufanya mchanganuo wa kibiashara. Pia niliwajibika kutoa ripoti za ndani na za nje kwa bodi ya kampuni.
Nini kilikuvutia ukachagua kazi hii?
Nilikuwa napenda hesabu tatizo sikuwa mzuri sana. Kwa kuwa nilikuwa napenda namba sana hivyo nikajua ndicho nacho paswa kusomea. Motisha ya Mama yangu ilinisaidia sana kufanya vizuri katika eneo nililopenda na muda ulivyozidi kwenda nikawa nafanya vizuri zaidi. Sekondari nilichukua masoma ya Fizikia na nikawa na nia ya kufanya kazi ya urubani. Muda mfupi baadaye nikaachana na ndoto hiyo kutokana na hofu ya kuwa angani.
Ilinibidi kuangalia kazi nyingine inayohusisha hesabu ndipo nikaingia kwenye uhandisi. Baada ya kumaliza masomo yangu ya kidato cha sita nilifanikiwa kupata udhamini wa masomo kwa wanawake waliofanikiwa zaidi kwa ajili ya masomo ya juu. Huo ndio ukawa mwanzo wangu wa kutimiza ndoto ya kuwa mhandisi.
Ni changamoto gani hukutana nazo kama mhandisi mwanamke na unaziepuka vipi?
Mara zote kwenye eneo la uhandisi wanawake ni wachache na ni dhahiri tangu nilipokua Chuo Kikuu na hata nilipoanza kazi Vodacom. Changamoto kubwa ilikuwa ni juu ya maoni ya wanaume ama niliosoma nao au kufanya nao kazi.
Pale nilipovaa gauni au sketi walikuwa wanasema sifanani kama mhandisi kwa kuwa awali nilipata hisia kuwa nawajibika kuvaa nguo mchanganyiko. Hata kwenye vikao maoni yangu hayakupewa kipaumbele kwa sababu ya mfumo dume. Mwisho nikaamua kupingana na vipingamizi. Hali hiyo ilinifanya kusikiliza na kuiamini sauti yangu ya ndani iliyopelekea kuona fahari kuwa miongoni mwa wanawake wachache katika fani ambayo wanaume ni wengi.
Nilizuia maoni hasi ambayo yaliyokuwa yana haribu kazi zangu au yanazuia uwezo wangu wakufanya kazi vitendo hivyo vilisababisha waanze kuheshimu kazi yangu.
Je, kuna njia yeyote mwajiri wako kakusaidia kuhimili vikwazo hivyo?
Nashukuru sana kwa ushirikiano wao waliounesha hadi nimefika hapa. Walinipa nafasi ya kusoma masomo ya shahada ya uzamili na pale nilipohitaji muda wa ziada kusoma waliniruhusu. Vodacom pia inatoa nafasi za semina na warsha mbalimbali kwa wanawake kwa ajili ya kujiendeleza na kujijengea uwezo kupitia mtandaoni na hata nje ya mtandao (offline) jambo ambalo limekuwa muhimu katika ukuaji wangu. Wanafanya hivyo kwa sababu ya kuwapa nafasi wanawake ili waweze kuonekana katika miradi na kwenye uongozi
Kuna umuhimu gani kuwasaidia wanawake wanaofanya kazi katika maeneo ya kampuni za simu au uhandisi?
Naamini wote wanaume na wanawake wana nafasi sawa katika eneo lolote lile. Pasipo shaka hata maeneo ya utendaji yanayotawaliwa na wanaume kama ya uhandisi wanawake wanahitajika kutoa mchango wao ili yapige hatua zaidi. Mfano, sisi wanawake huwa tuna sauti jikoni au ndani ya nyumba pale tunapotaka kuoana kwa kuhakikisha mpangilio wa sehemu hizo ni nadhifu. Tunahitaji hilo pia inapokuja kwenye kazi zetu. Ni imani yangu kila mtu ana jambo ya kuchangia katika maendeleo.
Kuwa na mchanganyiko wa wafanyakazi ni hatua kubwa kuelekea kwenye uguduzi na mafaniko ya kibishara. Unafikiri ni kwanini ushirikishwaji ni muhimu?
Ushirikishwaji ni lazima uwepo katika ofisi yoyote ile kuhakikisha kuwa wanaume na wanawake wanachukuliwa sawa. Isitokea hata mtu mmoja akanyanyaswa au akazuiwa kufanya kazi zake kwasababu ya jinsia yake, umri, dini, kabila au ulemavu. Kwa mfano, mwanamke anaweza kutokea katika familia ambayo mawazo yake hayaheshimiki au hayapewi kipaumbele lakini anapoondoka maeneo hayo na kwenda kuanza kazi, wanawajibu wa kuona mawazo yao yanakuwa ya muhimu na kuleta mabadiliko katika jamii.
Hali hiyo inafanya watu wajiamini kuhusu mawazo yao ambayo yanaweza kutatua matatizo yanayoikabili dunia kwa sasa.
Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwafanya wengine wajali kuhusu ushirikishwaji?
Ni ngumu kuweza kufikia ushirikishwaji kwa asilimia hibyo ni safari ambayo wote tunatakiwa kuichukua. Kama taasisi hakikisha kuna programu za kuelimisha kuhusu wafanyakazi wako kwenye dhana hiyo. Taasisi hiyo ihakikishe inawajibika na kuwa huru kufanya hivyo ili kubadilisha huo utamaduni, mawazo na imani isiyojali ushirikishwaji.

Pendo akifurahia jambo na wafanyakazi wenzie katika Ofisi Kuu ya Vodacom jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha zote kwa hisani ya Vodacom.
Unafikiri mwanamke anatakiwa afanye nini mahala pa kazi ili aweze kujiamini na kufanikiwa zaidi?
Wanawake wanatakiwa wajiamini katika nafasi zao na wasijutie maamuzi wanayofanya katika kuboresha maisha yao. Wanawake lazima wawe na nafasi ya kutafakari maisha yao wenyewe ili kujua njia ipi ni sahihi katika kazi zao na kisha kufanya uwekezaji huko au ubobezi katika maeneo hayo waliyoyagundua. Ushauri wangu wasiwe wanapokea ushauri wa kila mtu ila ule tu wa wafanyakazi wenzao na ukosoaji unaojenga wauchukilie kama fursa kwako. Waamini maono yao pia.
Umekuwepo Vodacom kwa muda sasa. Nini kilikufanya ujiunge nayo na kipi kimebadilika ndani ya kampuni hiyo kwa sasa?
Vodacom walikuja chuoni kwetu na kufanya usahili kwa wanafunzi na nilifanikiwa kushinda usahili ingawa sikutilia maanani. Nilianza kutilia maanani baada ya usahili na kugundua uhandisi utachukua nafasi kubwa katika kazi hiyo.
Nilipoanza wanawake walikuwa watatu tu na mimi nikiwepo katika idara yetu. Tulikuwa wachache sana sasa tumekuwa tukiongezeka hali hiyo inaonyesha Vodacom Tanzania ni kampuni inayosaidia ukuaji wa wanawake katika kazi na uongozi.
Soma zaidi kuhusu: Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania
Kigogo wa Safaricom kuiongoza Vodacom Tanzania
Mradi gani ulioupenda zaidi ndani ya Vodacom Tanzania ambao ni chachu ya ukuaji?
Mradi unaonivutia zaidi ulikuwa wa kuunganisha Net App ambao ulizinduliwa ndani ya kampuni ukiwa muhususi kwa jili ya kufuatilia utendaji kazi wa mtandao kupitia simu. Mradi huo ulisaidia kufanya maamuzi kutokana na ripoti za uhakika. Teknolojia hiyo ilisaidia kuongeza uwezo wa kujiamini katika kazi ambapo niliweza kuwasiliana na wafanyakazi wenzangu moja kwa moja jambo ambalo limeongeza mahusiano mazuri ndani ya kampuni.
Unaweza kuanisha mafanikio yeyote katika taaluma na maisha yako binafsi?
Ni mwanamke mwenye rekodi ya mafanikio binafsi na katika taaluma. Kufanikiwa kwangu kumetokana na kufanya kazi inayonihitaji zaidi bila kushuka, kuhitimu chuo kikuu katika ufaulu mzuri na bado nikabaki mama na mke. Ni mafanikio makubwa.
Takriban nusu (asilimia 47) ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania ni wanawake na asilimia 40 ya wajumbe wa Kamati Tendaji ni wanawake.
Kama mama na mke unaweza vipi kufanikwa vyote viwili familia na kazi inayokuhitaji zaidi?
Mwanzoni ilikuwa ngumu lakini ikanibidi kuchukua hatua zaidi ili kuweza kumudu hilo. Jambo la muhimu kuwa nikujitunza na kujali afya yangu na amani yangu. Hii ni kwa sababu kama sitaweza kujitunza mwenyewe sitaweza pia kuwatunza wengine. Nimepata ujuzi wa aina mbili ambao umenisadia kufanikiwa.
Moja ni nidhamu na ya pili ni uwezo wakufanya kazi zaidi ya moja. Nina ratiba toka asubuhi inayonifanya nifanye vizuri nikiwa kazini. Huwa naamka saa 10.30 usiku/afrajiri kila siku naandaa kifungua kinywa kisha natumia muda kidogo na familia katika mazungumzo ya asubuhi alfu tunasali kama familia.
Mume wangu na mimi huwa tunawapeleka watoto shule kabla ya kwenda kazini. Nahakikisha kuwa kila kitu nyumbani kiko sawa maana kama siyo hivyo nitashindwa kufanya kazi zangu za kila siku ofisini. Pia Napata msaada mkubwa kutoka kwa mama yangu na mume wangu. Mume wangu amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yangu. Naamni wanawake wanaweza fanya jambo lolote vizuri kuliko wanaume endapo watakuwa makini.
Umesema una watoto wawili mapacha, nini ndoto yako kwa watoto wakike hapa Tanzania?
Kama mzazi yoyote yule nina ndoto nyingi kwa watoto wangu na hasa kwasababu nina watoto wa wa kiume na wakike. Nataka wamjue Mungu, wawe na heshima na unyenyekevu na wenye malengo. Najua kuna chagamoto watakazo kutana nazo watakapozidi kuwa wakubwa lakini hasa kwa mtoto wangu wakike. Nataka mtoto wangu wakike awe chachu kwa wengine kwa mafanikio yake. Nataka yeye ajue anaweza kufanikiwa na kufanya chcochote anachopenda. Nawombea kwa Mungu mafanikio ya mbeleni wasichana wote wakitanzania.
Latest
