Zawadi ya Mark Zukerberg: Facebook kuwakutanisha makapela mtandaoni
- Mark Zuckerberg kuwaunganisha makapela zaidi ya milioni 200 wa Facebook, ikiwa ni huduma maalum tofauti na inayotumika sasa ya watu kutongozana ‘kienyeji’ mtandaoni.
- Makapela wa Bongo ni miongoni mwa wale watakaonufaika na huduma hiyo.
Wewe ni miongoni mwa wanaohaha kutafuta wachumba ukafikia kujaribu bahati yako hadi mtandaoni? Facebook wana mpango na wewe.
Katika kuimarisha mahusiano na wateja wake, Mtandao wa kijamii wa Facebook umezindua huduma mpya itakayowakutanisha makapela wanaotaka kuanzisha mahusiano ya ‘kimapenzi’.
Hatua hiyo imefikiwa na Facebook baada ya kubaini kuwa watumiaji zaidi ya milioni 200 wa mtandao huo walioandikisha taarifa zao muhimuni makapela (singles) na hawako kwenye mahusiano.
Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Facebook, Mark Zuckerberg alitangaza kuanza kwa huduma hiyo mwanzoni mwa wiki iliyopita na kueleza kuwa lengo lao ni kuimarisha mahusiano na wateja wake kwa kuwasaidia watu kutafuta wenza wa maisha.
“Ikiwa tumedhamiria kuwasaidia watu kujenga mahusiano yenye maana, basi hii (huduma) inaweza kuwa na maana kubwa,” alisema Zuckerberg na kuongeza kuwa huduma hiyo itawaweka karibu zaidi watumiaji wa mtandao huo ambao umepenya katika maeneo mbalimbali duniani.
“Tunaenda kujenga mahusiano ya muda mrefu,” alisema, “siyo tu kwa jili kujitangaza.”
Mwanzilishi wa Facebook na Ofisa Mtendaji Mkuu Mark Zukerberg akitambulisha rasmi huduma hiyo hivi karibuni. Picha ya Mtandao.
Taarifa za kutongozana zitakuwa siri
Hata hivyo, tofauti na baadhi ya watu waliopata wenza kupitia Facebook kwa kuwa tayari na urafiki nao, huduma hiyo haitawaunganisha wale ambao tayari ni marafiki kwenye mtandao huo badala yake itatafuta wengine ambao sifa zinashabihiana.
Huduma hiyo ya kutafuta wenza kwa Kiingereza ‘dating’ itakuwa inapatikana kwenye app ya Facebook ambapo haitaonekana kwenye wasifu wa mtu.
Watumiaji ambao ni makapela na wanapenda kutafuta wenza na kuanzisha mahusiano watatakiwa kutengeneza wasifu mwingine ndani ya akaunti zao za Facebook. Wasifu huo hautaonekana kwa marafiki au familia au kuonekana kwenye ukurasa wa kuingilia. Bali unaonekana kwa watu ambao wanatumia huduma hiyo ya kutafuta wenza.
Soma zaidi: Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
Facebook itakachokifanya ni kuwaunganisha watu na huduma hiyo kwa kuwataka wafungue makundi au matukio ambayo yatawawezesha watumiaji wengi wanaotafuta wenza kujiunga na makundi au matukio ya aina hiyo. Mtu ambaye hausiki na huduma hiyo hataweza kuona kinachoendelea kwenye makundi hayo.
Lengo ni kuhakikisha watu wanakuwa na mawazo yanayofanana ili kufahamiana na kujumuika pamoja(socialize) kwa ukaribu zaidi.Pia itawawezesha wateja kutuma ujumbe mfupi wa maneno ambao utatengenezewa ukurasa wake na hautahusiana na WhatsApp au Messenger.
Bado kuna maswali kibao
Hata hivyo, bado kuna maswali mengi ambayo Facebook inatakiwa kujibu hasa yale yanayohusu faragha na utendaji wa huduma hiyo. Kwa mfano, mtu yeyote anaweza kuanzisha mazungumzo? Nina uhakika kuna mengi ya kujifunza kuhusu huduma hii mpya Facebook.
Kwa wachambuzi wa masuala ya usalama mtandaoni wanasema hatua hiyo ya Facebook ni kujaribu kurudisha imani kwa wateja wake ikizingatiwa siku za hivi karibu ilikumbwa na kashfa kubwa ya kuvujisha taarifa muhimu za watumiaji wa mtandao huo.
Kashfa hiyo ilimuweka katika wakati mgumu, Zuckerberg kujisafisha kwa watumiaji wa mtandao huo ambao walianza kuhamasishana kuachana na Facebook wakidai siyo mahali salama.
Facebook sio mtandao wa kwanza kuanzisha jukwaa la mahusiano, ipo mitandao mbalimbali ambayo imekuwa ikitumika na watu kukutana na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi ambayo baadaye yanaweza kuhitimishwa kwa kufunga ndoa.
Hata hivyo, inashauriwa kutathmini faida na hasara za kutafuta wenzi au kuanzisha mahusiano mtandaoni ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufanya maamuzi ya kumpata mke au mme sahihi utakayeishi naye wakati wote wa uhai wako.
Hatua hiyo ya Facebook huenda ikawa ni lulu kwa makapela wa Tanzania ambao mtandao huo unakadiriwa kuwa na wafuasi wapatao milioni 6.1 hadi Desemba 2017 kwa mujibu wa mtandao wa Internet World Stats.