Watahiniwa zaidi ya 87,000 kidato cha sita kikaangoni leo

May 7, 2018 4:48 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link

Wanafunzi wakifanya mtihani katika moja ya shule za sekondari nchini. Picha ya Mtandao. 

  • Watakaofaulu mtihani huo wa Kidato cha Sita (ACSEE) watapata fursa ya kujiunga elimu ya juu katika vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini.
  • Idadi ya watahiniwa wa shule imeongezeka kwa asilimia 2.7 ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia watahiniwa 77,222 mwaka huu.
  • Idadi ya wanaume waliosajiliwa kufanya mtihani huo kama watahiniwa binafsi ni mara mbili ya ile ya wanawake.

Dar es Salaam. Wanafunzi 87,643 wa Kidato cha Sita nchini wameanza rasmi kutupa karata zao za mwisho zitakazobaini hatma ya safari yao ya kujiunga na elimu ya juu baada ya kuanza mitihani ya kuhitimu elimu hiyo leo.

Baraza la Mitihani (Necta) limetangaza kuanza kwa mitihani hiyo maarufu kwa kifupi cha Kiingereza (ACSEE) sambamba na ya Ualimu leo (Mei 7, 2018). Wanaofaulu vyema mitihani hiyo hupata sifa za kujiunga na elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu Tanzania.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles  Msonde amezitaka kamati zote za mitahani za mikoa, halmashauri, manispaa na majiji kuhakikisha taratibu za mitihani zinafuatwa ipasavyo.


Wahitaji kujua iwapo alama zako za mtihani wa kidato cha sita zinakuruhusu kujiunga na chuo kikuu? Tafuta majibu kwenye Elimu Yangu.


Katika mitihani huo, watahiniwa  wa shule mwaka huu wameongezeka kutoka 75,116 mwaka 2017 hadi kufikia watahiniwa 77,222 mwaka huu. Kati ya hao, wasichana ni 32,111 sawa na asilimia 41.5 ya watahiniwa wote.

Watahiniwa wa kujitegemea  wanaoketi katika mitihani hiyo ni 10,421 kati yao wanaume waliosajiliwa walikuwa 7,136, idadi ambayo ni takriban mara mbili ya ile ya wanawake.

Katika mitihani ya ualimu,  watahiniwa wa cheti na stashahada  wapato 7,422 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kupata ajira au kibali cha kufundisha iwapo watafaulu vyema. 

Dk Msonde amesema mtihani huo utafanyika katika shule za sekondari 674, vituo vya watahiniwa wakujitegemea 231 sambamba na vyuo vya walimu 125 kutoka bara na visiwani.

“Maandalizi ya mithani ya kidato cha sita na ualimu ya mekamilika ikiwamo kusambaza nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani hii,” amesema Dkt Msonde.

 

Enable Notifications OK No thanks