Fastjet yafanya mabadiliko makubwa huduma za vyakula, mizigo

August 6, 2018 7:43 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Huduma ya viburudisho ndani ya ndege pamoja na mteja kusafiri na begi la kilo 23 ni gharama itakayo kujumuishwa kwenye tiketi.
  • Tayari tiketi zilizoanza kuuzwa leo zinajumuisha mabadiliko hayo mapya.
  • Fastjet waeleza kuwa mabadiliko yataongeza nauli “ambazo abiria wataweza kuzimudu”.

Dar es salaam. Kampuni ya ndege ya Fast Jet imefanya mabadiliko katika utoaji huduma zake baada kuondoa utaratibu wa kuuza viburudisho ndani ya ndege katika safari zake ikiwa ni moja ya jitihada za kukabiliana na ushindani katika sekta ya anga barani Afrika.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa leo Jijini Harare, Zimbabwe, Fastjet pia haitatoza abiria wenye mizigo inayozidi kilogramu 23 tofauti na bei ya tiketi. 

Tofauti na awali ambapo abiria walikuwa wakinunua viburudisho na kulipia mizigo hiyo mbali na gharama za tiketi ya safari, taarifa ya Fastjet inaeleza kuwa sasa huduma hizo zitajumuishwa kwenye tiketi atakayokata mteja.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Fastjet, Nico Bezuidenthout  amesema “tumewasikiliza wateja wetu.” 

Bezuidenthout amesema uamuzi huo umechangizwa na utafiti uliofanywa kwa muda mrefu kwenye soko la usafri wa anga na wateja wake. 

Fastjet iliyoanza kufanya biashara mwishoni mwaka 2012 hufanya safari zake Tanzania, Zimbabwe, Afrika Kusini na Msumbiji.  

Mabadiliko hayo mapya yameshaanza kuonekana katika tiketi zake zilizoanza kuuzwa leo.

Makadirio ya bei ya safari ya ndege ya Fastjet kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya yakijumuisha gharama za viburudisho na mzigo usiozidi Kilogramu 23. Picha| Daniel Mwingira.

Mabadiliko hayo yameilazimu kampuni hiyo kufanya mapitio ya bei zake na kupandisha nauli ili ishabihiane na ubora wa huduma hizo kwa sasa.

Msemaji wa Fastjet nchini, Lucy Mbongoro ameiambia Nukta kuwa mabadiliko hayo sasa yataongeza gharama za tiketi ambazo zitakazoongezeka kwa kiwango ambacho “msafiri atakimudu”.

”Kutokana na mabadiliko hayo bado shirika letu litaendelea kutoa huduma kwa gharama nafuu ambayo mteja bado anaweza imudu na sasa bei hizo zitakuwa katika madaraja matatu ya nauli.

Mteja atayekata tiketi ndani ya siku 21 bei itakuwa ni tofauti na yule aliyekata siku 14 na saba kabla ya safari,” anaeleza Mbongoro.

Alipoulizwa iwapo uamuzi huo ni moja ya njia ya kukabiliana na ushindani, Mbongoro amekiri kuwepo kwa ushindani kwa sasa katika usafri wa anga Tanzania huku akieleza kuwa bado Fastjet ina uwezo mkubwa katika usafirishaji wa anga kutokana na hazina ya ndege mbili zenye uwezo wa kubeba abiri 104 kila moja huku wakifanya safari mara nne kati ya Dar na Mwanza. Kwa Tanzania kampuni hiyo ina ndege mbili aina ya Embrear 190.  

Fastjet imekuwa ikifanya mikakati mbalimbali ya kujiimarisha na kupunguza kiwango cha hasara. Ripoti ya Fedha ya Fastjet kwa mwaka unaoishia Desemba 2017 inaeleza kuwa kampuni hiyo ilipata hasara ya Dola za Marekani 24.5 milioni (Sh55.4 bilioni) ikiwa ni ahueni zaidi ya mara mbili kutoka hasara ya Dola za Marekani 67.7 milioni sawa na Sh153 bilioni iliyoripotiwa mwaka 2016. 

Ushindani katika sekta ya anga nchini unazidi kupaa baada ya Serikali kuendelea kuliimarisha Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) kwa kulikodishia ndege mpya ili kuongeza ufanisi. Hadi sasa Air Tanzania ina ndege tano ikiwemo Boeing 787-8 Dream Liner iliyoanza kufanya safari za majaribio mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro Julai 29 2018.

Enable Notifications OK No thanks