Vodacom yazindua teknolojia kudhibiti upotevu data za wateja

August 29, 2018 10:59 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Yazindua kifaa cha “Red Box” kitakachotumika kurejesha taarifa za wateja zilizopotea.
  • Kinapatikana katika maduka ya Mlimani City na Makao Makuu ya Vodacom Morocco Jijini Dar es Salaam.
  • Kina uwezo wa kutumiwa na simu 300 bila kuunganishwa na intaneti.

Dar es Salaam. Wewe ni miongoni mwa watumiaji wa simu za mkononi ambaye umepoteza data na kumbumbuku katika simu yako?Na huenda umetafuta suluhisho la kudumu lakini hujafanikiwa?.

Kampuni ya Vodacom Tanzania imezindua kifaa cha kidijitali kitakachotumiwa kuhifadhi na kurejesha data zilizopotea mara simu inapoharibika au kuibiwa.

Hatua hiyo ni sehemu ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara ambapo kifaa hicho cha kidijitali kinajulikana kama ‘Red Box’ kiko ndani ya duka katika Jengo la Makao Makuu ya Vodacom Morocco Jijini Dar es Salaam. 

“Maduka haya ya kwanza sokoni ya ‘zoni za kiteknolojia’ ni sehemu ya mkakati wetu wa kuhakikisha kwamba wateja wetu, ambao ndiyo kipaumbele chetu, wanapata huduma mwafaka na bora,” amesema Rosalynn Mworia, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Plc.

Duka hilo jipya litakuwa na vifaa vya kipekee vya zoni ya kiteknolojia ambapo wateja watahudumiwa kwa kutumia kifaa cha ‘Red Box’ ambacho kinaweza kutumika kuhamisha, kuhifadhi na kutunza data za mteja kama vile majina ya watu wa kuwasiliana nao, picha, muziki, video, ujumbe,  kalenda na Apps mbalimbali (Fabebook, WhatsApp, Instagram) kutoka simu moja ya kidijitali hadi kifaa kingine au kadi ya kumbukumbu (diski ndogo na diski mama) 

Kifaa hicho ambacho kinatajwa kama mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano kinapatikana pia katika duka la Vodacom la Mlimani City ambapo kinatumika kuhamisha data kwa kasi kubwa, hata bila kuwa kimeunganishwa na intaneti; ambapo kinaweza kutumiwa na hadi simu janja 300.

Teknolojia mpya ya ‘Red Box’ huenda ikawa suluhisho la kilio cha muda mrefu cha watumiaji wengi wa simu kupoteza data mara simu inapoharibika, kuibiwa au wakati wa kuhamisha.


Zinazohusiana:


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), Dk George Mulamula, ameipongeza kampuni ya Vodacom kwa jitihada zake katika kufanikisha Tanzania inakuwa ya kidijitali kupitia uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali zinazorahisisha mawasiliano. 

“Tunaishi katika dunia ambayo upatikanaji wa taarifa ni muhimu zaidi, hivyo kifaa hiki kinatuhakikishia kwamba taarifa zetu zitakuwa salama kupitia uhamishaji na urejeshaji wa taarifa mbalimbali,” amesema Dk Mulamula.

Dk Mulamula ambaye pia ni Mhandisi wa masuala TEHAMA, ameitaka  Vodacom kuhakikisha teknolojia hiyo mpya inasambazwa katika maduka yote nchini ili huduma hiyoiwasaidie Watanzania ambao wanakutana na matatizo ya kupoteza data.

Hata hivyo, bado Vodacom itakuwa na kibarua kigumu cha kuhahakisha ‘Red Box’  inakuwa sehemu ya kuhakikisha usalama, usiriwa taarifa na maudhui ya watumiaji wa simu za mkononi unazingatiwa.

Kampuni mbalimbali duniani ikiwemo Facebook imekuwa ikilaumiwa kwa nyakati tofauti kuvujisha au kutumia vibaya taarifa za wateja wake ilikujinufaisha kibiashara.

Mtaalamu wa usalama mtandaoni kutoka kampuni ya Kabolik, Robert Matafu amesema ili usalama wa taarifa mtandaoni; watumiaji wa wanapaswa kupewa uwezo wa kudhibiti wenyewe taarifa zao bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Enable Notifications OK No thanks