Tanzania kunufaika mkataba wa uhifadhi malikale, utamaduni
- Mkataba huo utaimarisha na kuendeleza ushirikiano uliokuwepo muda mrefu.
- Ni fursa ya kujitangaza kimataifa hasa katika sekta ya uhifadhi wa malikale.
- Utaimarisha ulinzi na matumizi sahihi ya rasilimali za nchi.
Dar es Salaam. Serikali imeendelea kubuni njia mpya za kutangaza na kukuza sekta ya utalii kimataifa kwa kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wa karibu na nchi zilizoendelea duniani ili kuvutia watalii wengi kuja nchini.
Leo 27 Agosti 2018, Serikali ya Tanzania na China zimesaini mkataba wa makubaliano ya miaka mitano ya ushirikiano wa kuhifadhi malikale na utamaduni wa mtanzania utakaorithishwa na vizazi vijavyo.
Akizungumza na Wanahabari mara baada ya kuweka saini kwenye mkataba huo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema mkataba huo ni mwendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu wa Tanzania na China na anategemea kuwa itakuwa ni fursa nzuri kutangaza na kukuza sekta ya utalii.
“Kwa kusaini makubaliano haya yataweza kukuza mahusiano kiuchumi na kijamii katika kutunza urithi wetu, na watu wataweza kupata elimu na ujuzi katika kuhifadhi na kusambaza taarifa za utalii,” amesema Hasunga.
Kupitia mkataba huo wa uhifadhi wa malikale, Tanzania itapata fursa ya kupata elimu na ujuzi kuhusu uhifadhi na uchimbaji wa masalia ya kihistoria na kubadilishana ujuzi na wataalam kutoka China.
“Wataalam wa Tanzania watapata nafasi ya kujifunza kuhusu urithi wa utamaduni kutoka China, maonyesho ya pamoja, semina mbalimbali za kutunza urithi wa dunia,” amesema Waziri wa Mambo ya Kale wa China, Liu Yuzhu.
Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga akisaini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika uhifadhi na Waziri wa Mambo ya Kale wa China, Liu Yuzhu. Picha| Lusungu Helela
Pia itakuwa ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii kwa sababu wageni kutoka China ndio wanaongoza kwa kutumia pesa za kigeni nyingi wakiwa kwenye shughuli za utalii nchini. Kulingana na Ripoti ya Utafiti ya Wageni wa Kimatiafa ya mwaka 2017 inaeleza kuwa watalii kutoka China hutumia kwa wastani wa Dola za Marekani 541 kwa usiku mmoja wawapo katika matembezi na sehemu za kulala wageni wakiwa nchini.
“Tunaweza kufanya mambo mengi katika sekta ya Utamaduni na utalii, kwasababu kila mwaka karibu wachina bilioni 1.3 hufanya utalii sehemu mbalimbali,” amesema Yuzhu.
Vilevile China ni mmoja ya nchi 15 zinazofanya mikutano ya kimataifa zaidi nchini ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia 17.9 huku ikitanguliwa na Uganda, Afrika Kusini na Kenya.
Kupitia mkataba huu wa ushirikiano, China imetoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuleta mawazo ya nini cha kufanya ili waweze kuendeleza sekta hiyo ya urithi wa malikale kwa vizazi vijavyo.
Wadau wa malikale wamesema makubaliano hayo yanatoa fursa ya kujifunza na kutangaza utalii katika mataifa makubwa na kuongeza Pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni na watalii watakaokuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
“Ni kitu kizuri kwasababu China na Tanzania wana mahusiano ya muda mrefu, na itatusaidia kupata wageni zaidi,” anaeleza Neema Mbwana, Muhifadhi wa malikale kutoka Idara ya Mambo ya kale.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa mkataba huo utabimarisha na kuboresha shughuli za ulinzi na uhifadhi wa malikale ili kujenga misingi ya usawa katika matumizi ya rasilimali za nchi.
“Ushirikiano huu utahusisha kutembeleana na mafunzo ya pamoja na pande zote mbili zitahusika katika ushirikiano katika urithi wa dunia,” amebainisha Meja Jenerali Milanzi.