BOT: Marufuku kurusha rusha hovyo noti
- Yasema haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuharibu fedha au sarafu ya Tanzania.
- Onyo hilo linakuja siku chache baada ya watu wawili kukamatwa wakidaiwa kuchezea na kukanyaga noti za Tanzania.
- Yabainisha kuwa mamlaka ya kuharibu noti na sarafu iko mikononi mwake.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imewataka wananchi kuheshimu fedha ya Tanzania kwa kuwa ni moja ya alama ya Taifa na kuonya kwamba kudhihaki na kukejeli noti na sarafu ni kosa la jinai.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii akiwaonyesha baadhi ya watu akiwemo Msanii wa muziki wa Bongo fleva, Maua Sama na mtangazaji wa kipindi cha runinga cha SHILAWADU, Soudy Brown wakichezea na kukanyaga pesa. Soudy na mwenzake walikamatwa na Polisi Septemba 15 tayari wametiwa nguvuni na polisi kujibu tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BOT, kuharibu noti au sarafu, au kuonesha dharau au dhihaka kwa noti au sarafu za Jamhuri ya Muungano ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu namba 332A cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Penal Code) Sura ya 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.
“Jambo hili ni dharau kwa serikali inayotumia gharama kubwa katika utengenezaji wa noti hizo'” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo kwa umma.
BOT imewatahadharisha wananchi kutokujihusisha na vitendo vya aina hiyo bali kuitunza fedha kama mojawapo ya tunu na alama muhimu ya uchumi wa nchi kwani noti na sarafu hizo zina alama muhimu inayolitambulisha taifa la Tanzania ambayo ni nembo ya Bwana na Bibi.
“Alama hii inapaswa kuheshimwa kama zilivyo alama nyingine kama Bendera ya Taifa. Utunzaji mzuri wa fedha zetu utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji,” Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BOT.
Muonekano wa noti ya Sh10,000 ambayo hutumika katika shughuli mbalimbali. Picha| The Citizen
Aidha, BOT imewataka wananchi kutunza pesa kwa kuwa ni mojawapo ya tunu na alama muhimu ya uchumi wa nchi ambapo utunzaji mzuri wa fedha utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji.
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha26 inaeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kutoa noti nasarafu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Noti na sarafu hizo zina alama muhimu inayolitambulisha taifa la Tanzania ambayo ni nembo ya Bwana na Bibi. Alama hii inapaswa kuheshimwa kama zilivyo alama nyingine kwamfano Benderaya Taifa,” inaeleza taarifa ya BOT.
Hata hivyo, taarifa hiyo imebainisha kuwa noti na sarafu zote zimetengenezwa kutoa thamani ya kisheria (legal tender) kama ilivyoandikwa juu ya noti au sarafu husika na pia BOT pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuharibu noti na sarafu.