Waziri Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini

October 3, 2018 7:19 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Changamoto inayojitokeza ni Tanzania kutumia takribani Sh100 bilioni kila mwaka kuagiza samaki, maziwa na nyama kutoka nje ya nchi licha ya kuwa na mifugo mingi.
  • Aapa kutekeleza maagizo na maelekezo yote ya Rais John Magufuli kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya uongozi wake mwaka 2020.
  • Changamoto kubwa iliyojitokeza katika ukoaji wa sekta mifugo na uvuvi ni mikopo hali iliyochangia sekta hiyo kuchangia asilimia 2.2 tu katika Pato la Taifa.
  • Sekta binafsi yaahidi kuipiga jeki wizara ya mifugo katika ujenzi viwanda nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesikitikishwa na kitendo cha Tanzania kutumia takribani Sh100 bilioni kila mwaka kuagiza samaki, maziwa na nyama kutoka nje ya nchi licha ya kuwa na ng’ombe takrbani milioni 30.5 na samaki tani milioni 2.7 walioko kwenye maziwa, mito na bahari bidhaa ambazo zingeweza kuzalishwa nchini na kuleta ajira na kujenga uchumi wa Taifa.

Mpina ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizindua Dawati la Sekta Binafsi la kusaidia sekta za mifugo na uvuvi linaloundwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ASPIRES kwa kushirikiana na SAGCOT, USAID pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambapo  amesema Serikali ya awamu ya tano haitakubali tena hali hiyo iendelee kwani mabilioni hayo ya fedha yangetumiwa hapa nchini yangechochea ukuaji wa viwanda na  uchumi.

“Mhe Rais amekuwa akihoji mara kwa mara kwanini tuagize samaki nje ya nchi, wakati tuna bahari, maziwa na mito yenye rasilimali nyingi?? Kwa nini  tuagize viatu na nyama kutoka nje wakati tunayo mifugo mingi inayotuzunguka?” amehoji Mpina na kuongeza kuwa,

“Kwa nini tumekuwa na viwanda vingi ambavyo havifanyi kazi maswali haya ya Mheshimiwa Rais ni maagizo na maelekezo kwa Wizara yangu ni lazima yapate ufumbuzi.”

Aidha, Waziri Mpina amesisitiza kuwa maagizo na maelekezo yote ya Rais Magufuli ni lazima yapatiwe majibu kwa vitendo kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya uongozi wake mwaka 2020.

“Tunaapa kutokushindwa na Mwenyezi Mungu atatusaidia. Hatutashindwa,” amesisitiza Mpina.

Amesema dawati hilo litakuwa daraja  baina ya wizara na sekta binafsi ili  kutoa suluhisho la changamoto zinikazoikabili sekta binafsi katika biashara na uwekezaji hali itakayoamsha na kuvutia uwekezaji wa viwanda nchini.  


Zinazohusiana:


Katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 ibara ya 25 a-q na ibara ya 27 a-p inaiagiza Serikali kufanya mageuzi katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji, thamani na masoko ya uhakika.

Mipango ya Serikali kutekeleza majukumu hayo imeainishwa katika  Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya pili (ASDP II) na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017-2020/2021 (FYDP II).

Rais Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 na hata baada ya kuchaguliwa ameahidi kufanya mageuzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi ambapo pia katika vikao na mikutano mbalimbali ameonyesha kutokuridhishwa na yanayoendelea katika sekta ya mifugo na uvuvi.

Katibu Mkuu anayesimamia Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid  Tamatama amesema changamoto kubwa iliyojitokeza katika ukoaji wa sekta mifugo na uvuvi ni mikopo hali iliyochangia sekta hiyo kuchangia asilimia 2.2 tu katika Pato la Taifa (GDP) ambapo kuanzishwa kwa dawati hilo kutasaidia kuinua sekta hiyo na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Dawati hilo litawaunganisha wadau na maafisa wabobezi katika mabenki, taasisi za fedha na biashara ndani na nje ya nchi na kutoa suluhisho la kiutawala na kifedha katika viwanda na maeneo mengine ya wawekezaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine amesema kuwa kwa sasa wavuvi na wafugaji wanakopesheka hivyo kupitia dawati hilo ni dhamira mageuzi ya haraka yatapatikana ikiwemo ujenzi wa viwanda na kutengeneza ajira nyingi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) akikagua  samaki aina ya pweza wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha TANIPESCA eneo la Kilindoni wilayani Mafia Septemba 24, 2016. Picha| Tanzania Daily Eye.

Enable Notifications OK No thanks