Dau la Bilioni 1 kutolewa kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Bilionea Mo Dewji

October 15, 2018 4:30 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Familia yaahidi kuwa mtoa taarifa pamoja taarifa zitabaki kuwa za siri kubwa baina ya mtoa taarifa na familia.
  • Waishukuru Serikali, taasisi za dini na vyombo vya habari kwa jitihada zinazofanyika kumpata Mo. 
  • Ni zaidi ya saa 85 zimepita tangu Mo atekwe katika hoteli ya Collesseum iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimepita zaidi ya saa 85 tangu kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (Mo Dewji) familia yake imejitokeza na kutangaza dau la Sh1 bilioni kwa mtu yeyote atakaetoa taarifa muhimu zitakazosaidia kupatikana kwake. 

Taarifa za awali kutoka Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa Mo mwenye miaka 43 alitekwa  Oktoba 11, 2018 na raia wawili wa kigeni wakati akiingia katika hoteli ya Collesseum iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam kwaajili ya kufanya mazoezi.

Akizungumza leo na wanahabari Msemaji wa familia, Azim Dewji amesema watatoa kiasi hicho cha fedha ili kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapatika mapema ili aendelee na majukumu yake. 

“Familia imapenda kutangaza zawadi nono ya Shilingi za kitanzania bilioni  moja (Tsh. 1,000,000,000) kwa yeyote atakaetoa taarifa muhimu zitakazopelekea kupatikana kwa mtoto wetu,” amesema Dewji. 

Amesema familia inaahidi kuwa mtoa taarifa pamoja taarifa zitabaki kuwa za siri kubwa baina ya mtoa taarifa na familia. 

Aidha, Msemaji huyo wa familia ya Mo ameishukuru Serikali na taasisi zake, vyombo vya habari na taasisi za dini kwa kazi kubwa ya kuutarifu umma na jitihada zinazofanyika katika kuhakikisha kwamba mtoto wao anapatikana mapema. 

“Tunashukuru taasisi za kidini na zisizo za kidini na kila mmoja wenu kwa maombi na kutufariji katika kipindi hiki kigumu familia inachopitia. Tunaomba muendelee kutuombea,” amesema.

Mtu yeyote mwenye taarifa za alipo Mo anaweza kuwasiliana na Murtaza Dewji ambaye mwanafamilia. 


Zinazohusiana:


Wakati huo huo, Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akiwa mkoani Arusha amesema Serikali inatarajia kusambaza kamera maalum za CCTV katika mikoa yote ya mipakani ili kuongeza ulinzi kwa raia na kuzuia matukio ya utekaji. 

“Matumizi ya teknolojia hayaepukiki katika dunia ya sasa, hivyo serikali tumejipanga tutaanza kutekeleza hivi karibu usambazaji wa kamera za CCTV katika miji mikubwa na mikoa iliyoko mipakani,” amesema Masauni. 

Masauni amesema Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi kuhakikisha matukio ya utekaji hayaharibu taswira ya nchini katika diplomasia ya kimataifa. 

Oktoba 13 mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alinukuliwa akisema mpaka sasa watu 20 wamekamatwa kwaajili ya kuhojiwa kufuatia kutekwa kwa Mo; tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia tajiri mdogo zaidi Afrika ambaye ana utajiri unafikia Dola za Marekani 1.5 bilioni (zaidi ya Sh3.42 trilioni)

Hata hivyo, Lugola aliwahakikishia Watanzania kwamba jeshi la polisi linaendelea kufanya kazi likishirikana na vyombo vingine vya usalama nchini kutekeleza wajibu wake licha ya ‘udhaifu wa hapa na pale’.

Alisema hofu ya kutekwa inastahili kuondolewa miongoni mwa wananchi, Jeshi la Polisi linaendelea kushughulikia na kuwa wanakusanya taarifa mbalimbali za kiintelijensia zinazohusiana na matukio ya utekaji watu.

Kwa mujibu wa Lugola, watu 75 wametekwa ndani ya miaka mitatu ambapo mwaka 2016 walitekwa 9 na mwaka uliofuata wa 2017 (27). Katika kipindi cha Januari hadi Oktoba, 2018 watu 21 walitekwa kati yao 17 walipatikana waki hai na wanne hawajapatikana hadi sasa.

 

Enable Notifications OK No thanks