Rais Magufuli atoa maagizo makali kwa wakuu wa mikoa, wilaya udanganyifu miradi ya maendeleo

Rais John Magufuli akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu (2018) leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha| Ikulu.
- Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari wanatakiwa kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.
- Pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika halmashauri 5 ambazo zimefanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na mwenge mwaka jana kutoonekana mwaka huu, wajieleze kwa kina kabla ya kuchukuliwa hatua.
- Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu wakimbiza mwenge walikuwa wakifanya ukaguzi wa kina wa miradi ya maendeleo ili kubaini ubora na manufaa ya mradi husika kwa wananchi.
- Katika mbio hizo miradi 1,432 yenye thamani ya Sh660.6 bilioni imezinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi, huku miradi 80 iliyopo katika halmashauri 64 ikikutwa na dosari mbalimbali.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.
Rais ametoa agizo hilo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu (2018) Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu wakimbiza mwenge walikuwa wakifanya ukaguzi wa kina wa miradi ya maendeleo ili kubaini ubora na manufaa ya mradi husika kwa wananchi.
“Mhe. Waziri Mkuu nataka yale maelezo ya kina watoe sasa, kwa nini wanadanganya Mwenge, kwa nini wanamdanganya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa Mwenge” amesema Rais.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika halmashauri 5 ambazo zimefanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na mwenge mwaka jana kutoonekana mwaka huu, wajieleze kwa kina kabla ya kuchukuliwa hatua.
Awali akitoa maelezo kwa Rais, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu wamefanya ukaguzi wa kina wa ujenzi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo jambo ambalo limerahisisha kubaini changamoto zilizojitokeza.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
- Rais Magufuli aingilia kati sakata la makontena ya Makonda
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama amesema katika mbio hizo miradi 1,432 yenye thamani ya Sh660.6 bilioni imezinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi, huku miradi 80 iliyopo katika halmashauri 64 ikikutwa na dosari mbalimbali.
Mhagama amebainisha kuwa dosari hizo ni pamoja na ubora hafifu wa miradi na kukosekana kwa uhalisia wa thamani ya mradi,pia walikagua miradi 94 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana na kubaini kuwa miradi 5 kati yake haifanyi kazi.
“Mhe. Rais tumeamua kuboresha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwatumia wakimbiza Mwenge kubaini ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma katika miradi pamoja na kuchukua hatua wakiwa hukohuko kwenye miradi” amesema Mhagama.
Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2018 ulianzia safari yake katika mkoa wa Geita Aprili 2 hadi 7 na kuzunguka mikoa yote 31 Tanzania na kuhitimishwa katika mkoa wa Tanga Oktoba 14 siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na wiki ya vijana kitaifa.
Latest