Vodacom, TCC, JTI zang’ara tuzo za waajiri bora Afrika

Moja ya sherehe zinazohusisha utambuzi wa waajiri bora katika sekta mbalimbali duniani iliyofanyika mwanzoni mwa Februari 2018. Picha| www.top-employers.com
- Kampuni hiyo imeshikilia nafasi hiyo kwa miaka mitatu mfululizo miongoni mwa kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano ya simu Afrika.
Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania imezidi kung’aa katika sekta ya mawasiliano baada ya kutajwa kama mwajiri bora Tanzania na Afrika kutokana na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyakazi wake.
Kampuni hiyo imeshikilia nafasi hiyo kwa miaka mitatu mfululizo miongoni mwa kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano ya simu Afrika.
Tuzo hiyo ya ubora imetolewa na taasisi ya The Global Top Employer ya nchini Netherlands ambayo inachambua na kutambua mchango wa waajiri katika kuhakikisha wanathamini hali za waajiriwa wao na jinsi vitengo vyao vya rasilimali watu vinavyofanya kazi.
Kampuni zingine zilizotunikiwa tuzo ya ubora ni pamoja na kampuni ya sigara ya Japan Tobacco International ya Tanzania (JTI Leaf) na kampuni ya sigara Tanzania (TCC) ambazo zimeshinda katika kipengele cha bidhaa na huduma.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Rasilimali watu kutoka Vodacom Tanzania, Perece Kirigiti amesema moja ya sababu iliyofanya kampuni hiyo kuwa mwajiri bora kwa mwaka 2019 ni kutokana na tathimini ya uchambuzi wa maswali 100 yaliyoulizwa kwa watu 600 kupitia mada 10 za masuala ya rasilimali watu.
“Hii ni heshima kubwa sana kwetu, kutambulika zaidi na inatufanya tuzidi kujikita katika kufanya vizuri na kuongeza utendaji wetu wa kazi,” amesema Kirigiti.
Zinazohusiana:Vodacom, Mastercard zaangazia biashara ya mtandaoni kupitia Virtual Card
NALA yaja na teknolojia ya kijanja kutuma, kupokea pesa
Vigezo vingine ni mchango na mikakati ya kampuni katika kuimarisha vipaji vya wafanyakazi, kuendesha biashara, dhana ya maendeleo na kujifunza teknolojia mpya na utoaji wa fidia na faida.
Licha ya taasisi hiyo kufanya kazi ya kutathmini mwenendo wa makampuni kwa muda wa miaka 25 sasa, inasaidia kuyajengea uwezo mashirika katika kukuza hadhi za waajiri, kujipima uwezo wa utendaji kwa kujilinganisha na kampuni nyingine duniani na kujifunza sera za kimataifa.
Vodacom Tanzania ambayo imepata hadhi ya kimataifa kuwa mwajiri bora, ni moja kati ya kampuni ya simu za mkononi zinazofanya vizuri katika kusaidia jamii kupitia taasisi ya Vodacom Foundation.