Rais Magufuli akutana na wanasiasa wa upinzani, Mfanyabiashara Rostam Aziz
- Rostam aipongeza Serikali uboreshaji wa miundombinu ikiwemo reli, barabara na bandari ambayo ni muhimu katika kuzalisha ajira na ukuaji wa uchumi.
- Wapinzani wamsifia Rais Magufuli kwa ujasiri na misimamo katika maamuzi ikiwemo utatuzi wa bei ya korosho.
- Wamuahidi kuendelea kumpa ushirikiano katika kutimiza ajenda za maendeleo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara Rostam Aziz pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu hali ya kisiasa na mwenendo wa shughuli za uchumi nchini.
Wanasiasa hao ambao wamekutana na Rais Magufuli leo (Novemba 13, 2018) Ikulu Jijini Dar es Salaam ni pamoja na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD) James Mbatia; Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa, John Shibuda; na Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Party (UDP), John Cheyo.
Baada ya mazungumzo hayo Rostam amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi bora na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo reli, barabara na bandari ambayo ni muhimu katika kuzalisha ajira na ukuaji wa uchumi.
“Tunamuunga mkono Rais kwa kuhakikisha watanzania tunawekeza katika nchi yetu, kukuza uchumi wetu, hilo ndilo la msingi kwa sisi wafanyabiashara,” amesema Rostam.
Kwa upande wake, Mbatia amesema kuwa Tanzania inafanya vizuri katika malengo 17 ya maendeleo endelevu, huku akibainisha lengo la elimu bora na shirikishi lipewa kipaumbele na akaeleza umuhimu wa kuwepo kwa umoja na upendo nchini.
“Watanzania wote wana kila sababu ya kuendelea kuijenga nchi yao kwa mawazo ya pamoja ya ujumbe uliopo katika wimbo wa Taifa, unaosisitiza amani, umoja na upendo,” amesisitiza Mbatia.
Zinazohusiana:
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage, joto la korosho likipanda
- Rais Magufuli ataja sababu za kuwafuta kazi Dk Tizeba, Mwijage
Vilevile Shibuda amempongeza Rais Magufuli kwa hatua alizozichukua katika utatuzi wa soko la korosho na kumhakikishia kuwa vyama vya siasa vinamuunga mkono katika kurekebisha dosari na mmomonyoko wa maadili ndani ya serikali na vyama vya siasa.
“Rais Magufuli amerejesha sifa ya utaifa wetu ya kuwa nchi ya kuaminika na kusadikika na amekweza hali ya uhuru na kujitegemea,” amesema Shibuda.
Naye Cheyo hakuacha kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwa na moyo wa ujasiri katika kuchukua maamuzi magumu katika miaka mitatu ya uongozi wake tangu alipoingia madarakani mwaka 2015.