Majaliwa: Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache

December 5, 2018 7:08 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi.
  • Onyo la Majaliwa linakuja ikiwa zimepita siku mbili tangu alipowatahadharisha mawaziri na viongozi wengine Serikalini kutumia mitandao hiyo vizuri ili kuepuka mambo ambayo jamii haikubaliani nayo.
  • Amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Tehama ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amewaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache na kutaka mitandao hiyo itumike kuhamasishana mambo mema ikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali.

Amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano (Tehama) kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la  kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Onyo la Majaliwa linakuja ikiwa zimepita siku mbili tangu alipowatahadharisha mawaziri na viongozi wengine Serikalini kutumia mitandao hiyo vizuri ili kuepuka mambo ambayo jamii haikubaliani nayo.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam (Desemba 5, 2018) katika sherehe za utoaji tuzo za  Tehama zilizoandaliwa na kampuni ya simu ya Huawei ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini na kusema kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote kulingana na sheria zilizopo.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi,” amesema Majaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali inaamini kuwa matumizi ya Tehama yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja. 

Makosa yote ya mtandaoni ikiwemo mitandao ya kijamii yanashughulikiwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 chini ya kanuni za Maudhui ya Mtandao za mwaka 2018 (Electronic and Postal Communications (Online Content) Regulations 2018).  

Kanuni hizo zinaongeza nguvu juu ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa utekelezaji wake unadhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji nchini.

Tangu zilipopendekezwa mwaka jana, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu walijitokeza na kuhoji baadhi ya vipengele ambavyo vilionekana kukiuka faragha za watu, kuminya uhuru wa wananchi kujieleza na kutoa maoni.  

Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wana uwezo wa kuwalazimisha watumiaji na wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12 na kama hawajatimiza maagizo hayo wanaweza kulipa fidia isiyopungua milioni tano  au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.


Zinazohusiana: 


Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya Tehama ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku. 

“Matumizi ya Tehama kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi,” amesema Majaliwa.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya Tehama ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Amesema kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ina uwezo wa kuona na kubaini makusanyo yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi kinachoingizwa benki kwa kupitia tehama.

Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za sekondari, ofisi za wakuu wa wilaya, polisi, hospitali za wilaya, vyuo vikuu na vituo vya posta.

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amekihutubia wakati wa kukabidhi tuzo za Tehama zilizoandaliwa na kampuni ya Huawei leo Jijini Dar es Salaam. Picha| Michuzi.

Wakati huo huo, ameipongeza kampuni ya Huawei kwa uzinduzi wa programu yao ya “Seed of the Future” ambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa tehama wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa. 

Iwapo tehama itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.  

Mashindano hayo yaliasisiwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano hayo. 

Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu, wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini. 

Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Balozi Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania, Frank Zhou na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa nchini.

Enable Notifications OK No thanks