Matumaini makubwa kuzaliwa mji wa Silicon Dar

January 3, 2019 2:27 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link

Eneo hili lililopo jijini Dar es Salaam ndiyo linatajwa kuwa kitovu cha shughuli za teknolojia kutokana na kusheheni kwa makampuni mbalimbali zikiwemo za simu na vituo atamzi. Picha| SkyscraperCity.


  • Unapatikana kando kando mwa barabara ya Old Bagamoyo na Ali Hassan Mwinyi na maeneo ya jirani hasa Morocco, Victoria na Makumbusho ambayo yana kampuni nyingi za teknolojia.
  • Wadau waiomba Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa eneo hilo ili kuwavutia wengi zaidi.
  • Ni wakati wa kampuni ndogo za teknolojia kuanza kuangalia uwezekano wa kuhamia katika eneo hilo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa teknolojia huwezi kukwepa kusikia mji wa ‘Silicon Valley’ ndani ya Jiji la California nchini Marekani. Wabunifu kutoka katika maeneo mbalimbali duniani wanatamani kufika katika mji huo ili kujifunza na kupata ujuzi kutokana na uwepo wa kampuni na vituo vingi vya kijamii vya kuendeleza ujasiriamali na teknolojia.

Hapo ndiyo kuna makao makuu ya kampuni ya Google, Facebook, Apple na nyinginezo ambazo zinatumia teknolojia hasa ya mawasiliano na habari kutatua changamoto zilizopo katika jamii. 

Lakini mji huu huenda ukahamia Jiji la Dar es Salaam kando kando mwa barabara ya Old Bagamoyo na Ali Hassan Mwinyi na maeneo ya jirani hasa Morocco, Victoria na Makumbusho. 

Eneo hilo limeanza kujipatia umaarufu kutokana na kuwepo kwa majengo marefu ya kifahari ambayo yanatumiwa na kampuni za teknolojia zikiwemo za mawasiliano ya simu kama Vodacom, Tigo, Halotel na Airtel. 

Pia kunapatikana vituo vingi vya kijamii na atamizi za kukuza ubunifu wa teknolojia, ujasiriamali ikiwemo Buni hub, Sahara Ventures,  Atamizi ya Biashara na Teknohama (DTBi), Smart Lab, SeedSpace wakiongozwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).


Zinazohusiana: Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua

                           Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018


Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanaeleza sababu mbalimbali zilizofanya eneo hilo kujipatia umaarufu kiasi cha kuvutia makampuni kuwekeza mitaji yao ili kutoa huduma na kutengeneza ajira kwa watu. 

Mtaalam wa wa kujitegemea wa programu za kompyuta, Joshua Mabina anasema mfumo wa ufanyaji biashara na utoaji huduma za teknolojia unalazimisha kampuni nyingi kukaa sehemu moja ili kuwavutia wateja wengi kupata huduma za uhakika.

 “Watu hasa wanaojihusisha na teknolojia ya Tehama wanahitaji eneo la biashara na kuwa karibu na watu wanaofanya vitu kama vyao,” amesema Mabina.

Eneo hilo pia liko karibu na ofisi za Serikali na mashirika ya kimataifa ambayo yana uhusiano wa karibu na shughuli za teknolojia ambazo zina mchango mkubwa katika maendeleo ya watu na Taifa. 

“Hili eneo ni muunganiko kutoka maeneo kama Masaki, Oysterbay na kwenda Posta na kuna watoa maamuzi wengi kwenye taasisi na mashirika mbalimbali hivyo kuwa nao karibu ni fursa,” amesema Paul Madela msimamizi wa kituo cha Buni Hub.

Madela amesema kuna uwezekano mkubwa wa eneo hilo kuwa kitovu cha teknolojia kama litaendelezwa na kuboreshwa jambo ambalo litavutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika maeneo muhimu ya maendeleo.

                   

Hata hivyo, kukua kwa mji huo kunategemea uboreshaji wa sera na sheria zinazosimamia ukuaji wa sayansi na teknolojia katika jamii ili kuwavutia vijana kubuni njia rahisi za kutatua changamoto za jamii. 

“Sheria na sera za nchi ziwe vizuri na zitoe nafasi kwa wabunifu wa teknolojia kufanya kazi,” amesema Given Edward mwazilishi wa programu tumishi ya simu ya Mtabe.

Wawekezaji ambao wameanza kutumia fursa ya uwepo wa majengo marefu na miundombinu iliyopo katika eneo hilo wanasema matumaini ni makubwa kwa eneo hilo kuendelezwa na kuwa mji rasmi utakaotambulika kama sehemu ya kukuza ubunifu na teknolojia. 

“Tumekuja kuwekeza eneo ambalo linaweza kuwa mji wa Silicon kwa Dar es Salaam kwasababu tuna uzoefu na kufanya kazi na wajasiriamali wa teknolojia,na uhitaji ni mkubwa” amesema Innnocent Mallya, Meneja Mkuu wa kituo cha SeedSpace Tanzania.

Mwaka 2018, Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), iliipatia Tanzania msaada wa Sh77.3 bilioni  kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, ili kupunguza masongamano wa magari.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3 Itahusisha ujenzi wa barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa awamu ya nne ya ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).

Uboreshaji wa miundombinu utasaidia kuling’arisha eneo hilo na ikizingatiwa kuwa barabara hiyo ina msongamano mkubwa wa magari  ambapo kwa siku moja takribani magari 52,000 hupita kwenye barabara hiyo.

Enable Notifications OK No thanks