Meli mpya Ziwa Victoria kuchochea biashara Afrika Mashariki
- Itaziunganisha bandari za Tanzania, Kenya na Uganda huku ikiongeza usafirishaji wa abiria na bidhaa katika ukanda huo.
- Inajengwa na kampuni ya Hispania ya SENER na GAS Entec ya Korea Kusini.
- Itakuwa na urefu wa mita 90, itabeba abiria 1,200, mizigo tani 400 na magari 20 kwa wakati mmoja.
Dar es Salaam. Licha ya bandari za Dar es Salaam na Mombassa ya Kenya kuwa viunganishi muhimu vya biashara inayofanyika ukanda wa Afrika Mashariki, lakini huenda ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria utachochea zaidi ukuaji wa biashara katika eneo hilo.
Afrika Mashariki ina njia kuu mbili za biashara. Mlango wa kaskazini unaanzia bandari ya Mombasa ikipitia Uganda mpaka Rwanda, Burundi na Congo (DRC), na kuunganisha nchi za Sudan ya Kusini na Ethiopia. Mlango wa pili unaanzia katika bandari ya Dar es salaam kwenda Rwanda, Burundi na eneo lote la Maziwa makuu.
Hatua hiyo itafikiwa baada ya kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuingia mkataba na kampuni mbili za SENER na GAS Entec kujenga meli kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 itakayokuwa inafanya shughuli zake katika Ziwa Victoria.
Meli hiyo itakayokuwa na urefu wa mita 90 na uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo na magari 20 itakuwa ni meli kubwa zaidi katika ziwa hilo.
Kampuni ya SENER ya Hispania iliyobobea katika uhandisi na teknolojia itahusika na usanifu na michoro ya meli hiyo ambayo itaunganisha bandari za Kenya, Tanzania na Uganda ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji abiria na bidhaa.
Vifaa vya meli hiyo vinatengenezwa na kampuni ya GAS Entec yenye makao yake Korea Kusini na vitasafirishwa hadi mkoa wa Mwanza kwajili ya kuviweka pamoja na kujenga meli hiyo ambayo bado haijapewa jina.
Mchoro wa meli mpya itakayojengwa na kampuni za SENER na GAS Entec ambapo kukamilika kwake kutachochea biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi mwishoni mwaka 2018 alisema meli hiyo itajengwa kwa miezi 24 na kuondoa changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika eneo la maziwa makuu.
Ujenzi wa meli hiyo unaenda sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ambayo itaongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo inayoingia katika nchi za Uganda, Burundi na Rwanda.
Zinazohusiana:
- Zanzibar, kitovu utengenezaji wa meli Afrika Mashariki
- Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai
- Rais Magufuli atangaza siku nne za maombelezo ya waliofariki katika ajali ya Mv Nyerere
Meli mpya itakuwa ya aina yake
Kwa mujibu wa kampuni ya SENER ambayo ni msanifu mkuu, meli hiyo itajengwa kwa vyuma na itawekewa pangaboi (double screw propeller) mbili ambazo zitaendeshwa na injini mbili za ndani.
Pia itakuwa na vifaa mahususi vya kudhibiti upepo wakati wa safari na chombo maalum (Aft cargo) kwa ajili ya kupanga na kuhifadhi magari na mizigo.
Itakuwa na milango mikubwa miwili; mmoja wa kupitisha magari na mwingine mdogo unaonganishwa na barabara ya kupitisha mizigo hadi katika eneo la kuhidhia.
Juu ya staha kuu (deck) kutakuwa na staha nne kwa ajili ya abiria na wafanyakazi. Chini ya staha kuu ya injini moja kwenye eneo la ‘aft’ kutakuwa na msaidizi wa mashine na nafasi moja ya chupa ya upinde ambayo itawekwa mbele ya meli.
Pia itakuwa na eneo la malazi, jenereta la dharura na mfumo wa kuongoza meli ambao utakuwa katika staha ya juu.
SENER yenye uzoefu wa kujenga meli zaidi miaka 60 inasema meli hiyo itakuwa na ufanisi mkubwa wa kutoa huduma za majini kwasababu mfumo wake ni wa kisasa kukabiliana na changamoto za ufundi zitakazojitokeza.
Septemba 3, 2018, Rais John Magufuli alishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi meli hiyo mpya na ukarabati wa meli mbili za MV Victoria na MV Butiama na chelezo kitakachotumika katika ujenzi na ukarabati wa meli hizo.