Serikali yapiga ‘stop’ biashara ya wanyama pori nje ya nchi
- Imesema iko mbioni kufanya mabadiliko ya sheria ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena.
- Wananchi wanaofuga wanyama pori vikiwemo vipepeo wameshauriwa kuvitumia kama vivutio vya utalii ili kujipatia kipato.
Dar es Salaam. Wewe ni mfugaji wa wanyama pori? Na una mpango wa kuwauza nje ya nchi ili kujipatia kipato kuendesha maisha yako? Basi fahamu kuwa Serikali imetoa muelekeo mpya wa biashara hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema kwa sasa Serikali haitoruhusu tena biashara ya usafirishaji wa wanyama pori hai nje ya nchi na inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuhalalisha zuio hilo.
Amewataka wananchi wanaofuga wanyama pori waangalie namna nyingine ya kufaidika na biashara hiyo ikiwemo kuwatumia katika shughuli za utalii ili kujipatia kipato.
Tamko hilo limetolewa leo (Februari 8, 2019) bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab aliyetaka kujua ni lini Serikali itawaruhusu wananchi wa kijiji cha Fanusi wilayani Muheza kusafirisha vipepeo nje ya nchi baada ya kuzuiwa kwa miaka mitatu?
Kabla ya Dk Kigwangalla kutoa majibu yake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema vipepeo ni moja ya aina ya wanyama pori waliokuwa wakisafirishwa nje ya nchi kwa mujibu wa Sheria ya KuhifadhiWanyama namba 5 ya mwaka 2009.
Kutokana na wafanyabiashara kukiuka sheria na kanuni zake, Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyama pori hai nje ya nchi kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Mei mwaka 2016.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alipotembelea moja ya shamba la vipepeo katika tarafa ya Amani jijini Tanga mwaka jana ambapo aliwataka wafugaji hao kutumia fursa hiyo kama bidhaa ya utalii. Picha|Mtandao.
Balozi Rajab hakuridhishwa na majibu ya Kanyasu alisimama kuuliza swali la nyongeza ambapo amesema zuio la Serikalililihusu wanyama wakubwa na siyo vipepeo ambao ni wadudu huku akiitaka kuwasaidia wananchi wa Fanusi ambao wanakosa mapato yatokanayo na vipepeo.
Ndipo aliposimama Dk Kigwangalla na kutoa ufafanuzi kuwa Serikali itaendelea kuzuia biashara ya usafirishaji wanyama hai nje ya nchi na iko katika mchakato wa kufanya mabadiliko ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena nchini.
“Ninaomba kuweka sawa rekodi ifuatayo kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa sasa hatutoruhusu tena usafirishaji wa wanyama hai kutoka nchini mwetu kwenda nchi yeyote ile.
“Kwahiyo huo ndio uelekeo waondokane na mentality (fikra) kwamba kuna siku tutafungulia vibali vya kusafirisha nje ya nchi kwa sababu tumezuia na hatatufungua tena,” amesisitiza Dk Kigwangalla.
Zinahusiana:
Amesema ni vema wananchi waangalie fursa zingine za kufaidika na rasilimali hiyo ya wanyama pori kuliko kutegemea kusafirisha nje ya nchi.
“Utaratibu ambao tunaushauri kwa wananchi wote ambao walikuwa wakifuga hawa wanyama pori watafute namna nyingine ya kupata faida kutokana na maliasili hiyo na siyo kutegemea kusafirisha kwenda nje ya nchi,” amesema.
Akizungumzia suala la biashara ya vipepeo, amesema anatambua hadha wanayopata akina mama wa kijiji cha Fanusi tangu walipokatazwa kusafirishwa wadudu hao na kuwataka watumie njia nyingine ya utalii kupata mapato.
“Wakina mama pale Fanusi niliwashauri Halmashauri washirikiane na TFS (Wakala wa Misitu) kutafuta namna ya kufanya shughuli ya utalii wa vipepeo katika eneo lile kwa sababu vipepeo waliopo pale ni wazuri mno na watu wangeweza kwenda kuwaona lakini ingekuwa ni kivutio cha utalii wangepata kipato ambacho walikuwa wanakitarajia,”