Huyu ndiye muuza biriani kidijitali Dar
- Hutumia mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook na Instagram katika kujitangaza kibiashara.
- Awashauri wajasiriamali kutumia rafiki zao wa karibu katika kujitangaza na kujipatia wateja.
- Anatamani siku moja biriani lake livuke mipaka ya Tanzania.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mkazi wa Dar es Salaam na upo katika mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook au Instagram na mpenzi wa kula biriani unaweza ukawa umesikia au kuona Mudi Mabiriani katika pita pita zako.
Lakini je, ulishawahi kujua safari yake kwa ujumla na ameleta jambo gani jipya katika biashara ya chakula?
Nukta tunakuletea safari ya Mohammed Ahmed (35) maarufu kama Mudi Mabiriani kijana anayejihusisha na ujasiriamali wa vyakula hasa biriani na pilau pishori Jijini Dar es Salaam ambaye anatumia zaidi mitandao ya kijamii katika kutangaza biashara yake.
Matumizi ya teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano katika biashara yake ni moja ya vitu vinavyofanya biashara yake ionekane ya kibunifu zaidi tofauti na wapishi wengine wa chakula hicho kilichozoeleka zaidi ukanda wa Pwani wa Tanzania.
Kabla ya kuwa mjasiriamali wa biriani alianza kufanya kazi katika hoteli mbalimbali ndani na nje ya nchi mpaka alipoamua kuacha kazi na kujiajiri mwenyewe kwa kuanzia mtaji wa Sh100,000 tu.
Moja ya chakula kinachopikwa na Mudi Mabiriani katika shughuli zake za kila siku. Biriani ni chakula ambacho kinachowavutia watu wengi kwa sasa hususan siku ya Ijumaa. Picha| Mudi Mabiriani.
“Nilianza kwa kuwatumia rafiki zangu meseji za kawaida kuwa nauza biriani, kabla sijaanza rasmi kutangaza kokote,” anasema Mudi Mabiriani.
Hata hivyo, imezoeleka sana kwa watu wengi kipindi cha nyuma kuwa wanaouza biriani ni wanawake au wanaume watu wa makamo lakini Mudi Mabiriani, kijana mtanashati, ameweza kufuta hiyo dhana ya kuwa vijana hawawezi kupika au kuuza chakula.
Mudi mabiriani ameiambia Nukta kuwa alijifunza kupika biriani na viungo vyake kutoka kwa mama yake na baada ya kumudu pishi hilo kwa mara ya kwanza aliuza sahani 30 lakini wengi wa wateja wake wakiwa ni marafiki zake.
“Kwa wajasiriamali wanaochipukia nawashauri watumie mitandao ya kijamii na wawafanye rafiki zao kuwa wateja hata wanaweza wasije wao ila wakatumia wengine,” amesema Mudi Mabiriani.
Pamoja na hayo Mudi Mabiriani ambaye kwa sasa anauza zaidi ya sahani 200 za biriani siku za ijumaa, ameweza kuwafungulia milango ya ajira kwa vijana zaidi ya 10 ambao wanamsaidia katika kuuza biriani au kupeleka oda sehemu mbalimbali kwa wateja wake.
Zinazohusiana: Wajasiriamali wafundwa njia za kupata mitaji
Wanawake msisubiri kubebwa fursa za teknolojia – Wadau
Uwepo wa wateja wa kuwapelekea kwa wateja anaowafahamiana tayari, haikumnyima nafasi ya kuingia katika mitandao zaidi ambapo mpaka sasa amejiunga na mtandao wa Jumia na Misosi Hub ili mteja aweze kuoda biriani mtandaoni.
“Ukiondoa hapo pia huwa nashirikiana migahawa mingine kama saba mimi napeleka biriani na wao wanauza vyakula vingine,” anasema..
Kwa wastani Mudi Mabiriani huuza biriani lake kati ya Sh6,000 hadi Sh7,000 kwa sahani lakini kwa wale wanaohitaji kupelekewa chakula chao hutakiwa kulipia gharama za ziada za usafiri wa wastani wa Sh3,000 kwa maeneo ya Kariakoo, Masaki na mitaa ya mbali kutoka Sinza kama Kinyerezi hutakiwa kulipia hadi Sh5,000 zaidi ya bei ya wastani.
Hata hivyo, anatakiwa kukabiliana na kadhia kadhaa za Dar es Salaam kama foleni, ukosefu wa anuani rafiki za mitaa na utapeli kwa baadhi ya wateja.
“Kuna changamoto lukuki tunakabiliana nazo ikiwemo wateja kuchanganya oda mfano anataka biriani kuku lakini akifika kule anabadilisha kuwa alitaka biriani nyama. Pia, baadhi ya wateja huwa wanahama kutoka mahali alipoomba apelekewe chakula na kusababisha chakula kirudishwe,” anasema.
Ili kukabiliana na foleni ya Dar, Mudi anaeleza kuwa hutumia bodaboda na kampuni ya uchukuzi katika kuwasilisha bidhaa hizo kwa wateja wake.
Kasi yake ya kufanya masoko mtandaoni imeamsha vijana wengi au kina dada wengi kuanza kuuza biriani katika maeneo tofauti jijini hapa. Usishangae na majiji mengine kama Mwanza, Arusha na Mbeya kukawa na huduma hizo ambazo mteja huagiza mtandaoni na kupelekewa hadi nyumbani kwake.
Mudi Mabiriani ukiondoa kujiingiza kwenye mitandao vilevile amefanikiwa kuwafundisha vijana wengine sita namna ya kupika biriani na kujiajiri wenyewe.
Hii ni kutokana na kuona kuna umuhimu mkubwa kwa vijana kufanya kazi kwa kujiamini na kujifunza kwa wengine ili waweze kuendelea na kujipatia riziki halali.
Alipoulizwa na Nukta kama ana mpango wa kuanzisha App yake siku za usoni, amesema kuwa yupo mbioni kufanya hivyo lakini kwa sasa anajitangaza zaidi kwenye mitandao ya kijamii na kuimarisha soko lake.