Atiman House: Moja ya maghorofa matano ya kwanza kujengwa Dar lililoficha historia lukuki

February 16, 2019 2:16 pm · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Lilijengwa miaka 153 iliyopita na limefanyiwa ukarabati ili liendelee kudumu muda mrefu ujao.
  • Atiman House ni jina la Katekista Dkt Adrian Atiman aliyekombolewa utumwani nchini Mali.
  • Jengo hilo lilinuliwa na Wamisionari wa Afrika mwaka 1921 kutoka kwa mpiga picha wa Kiingereza.
  • Ni kivutio kikubwa kwa watalii kutokana na mwonekano na malighafi zilizotumika kulijenga.

Dar es Salaam. Bado tunaendelea la safari yetu ya kuchimbua historia ya Jiji la Dar es Salaam hasa ujenzi wa majengo ya mwanzo kabisa wakati huo ikijulikana kama Mzizima yanayotoa taswira halisi ya muonekano wa sasa wa jiji hilo.

Kando ya Barabara ya Sokoine ambayo ni maarufu kuingia katikati ya jiji kutoka maeneo ya Mbagala na Kariakoo unakutana na jengo la Atimani House moja ya maghorofa matano ya mwanzo kabisa kujengwa Dar es Salaam.

Jengo hilo lenye ghorofa moja liko mita 300 tu kutoka lilipo ghorofa la kwanza kujengwa katika jiji hilo la  ‘Old Boma’  ambalo liko chini ya usimamizi wa  Kituo cha Urithi wa Ubunifu Majengo jijini Dar es salaam (DARCH).

Ghorofa hilo la rangi nyeupe la  Atiman House, lenye madirisha membamba likisadifu mtindo wa kizamani, kwa sasa lipo mkabala na kituo cha mabasi ya yaendayo haraka (DART) cha Posta ya Zamani.

Atimani House linalomilikiwa na Shirika la Wamisionari wa Afrika  lilijengwa mwaka 1866 ikiwa ni miaka sita tu tangu lilipojengwa ghorofa la kwanza jijini hapa la Old Boma.

Kwa wanaotumia barabara ya Sokoine hawawezi kutambua kirahisi kuwa ghorofa hilo ni la muda mrefu kwasababu limefanyiwa ukarabati mkubwa ili kulifanya liendelee kuishi lakini limebaki na mwonekano wake wa zamani.


Soma zaidi: Lijue ghorofa la kwanza kuengwa Dar


Lakini ili uweze  kuingia ndani ya ghorofa hilo lazima ubonyeze  kengele iliyopo mlangoni kwa ajili ya kupata ruhusa ya kukutana na wasimamizi wa jengo hilo. 

Kwa unayesaka historia ya ghorofa hilo utaikuta kwenye picha na maelezo yaliyobandikwa kwenye kuta za jengo hilo, ambazo zitakurudisha miaka ya 1860 wakati huo Dar es Salaam ikijulikana kama Mzizima.

Katika moja ya maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiengereza yanamnukuu Mwanahistoria  Paul Foster ambaye ni Mkufunzi kutoka Chuo KIkuu cha Makerere cha Uganda akieleza kuwa  ghorofa hilo lilikuwa maalum kwa makazi ya wanawake (mahawara ) wa Sultani Majid bin Said.

Lilifikaje katika mikono ya Wamisionari wa Afrika?

Atimani House lilikiwa ni moja ya majengo matano yaliyojengwa na Sultani Majid bin Said kabla ya kifo chake mwaka 1870 pia kama Old Bona kwa sehemu kubwa limejengwa kwa  kutumia matumbawe (Coral reef), miti ya ‘mangrove’ (mikoko) pamoja na chokaa ambayo ni malighafi zinazopatikana bahari.

Jengo hilo lenye miaka 153 mpaka sasa lilichukuliwa na Wajerumani baada ya mgawayo wa bara la Afrika, lakini umiliki wake ulibadilika  mara tu baada ya vita ya kwanza ya dunia mwaka 1918 na kuwa chini ya himaya ya Mwingereza.

Maelezo yaliyobandikwa katika kuta za jengo hilo yanabainisha kuwa Atimani  House lilinunuliwa na Wamisionari wa Afrika kutoka kwa mpiga picha wa kiingereza ambapo walikabidhiwa rasmi Juni 10, 1921. 

Mwezi mmoja baadaye yaani Julai 27 mwaka huo huo, lilipata baraka na kuanza kukaliwa na Padri wa kwanza wa shirika hilo, Padri Joseph Laane na Bruda Jean.

Moja picha ya Askari wa Kijerumani wakipita mbele ya jengo la Atiman House iliyopo katika jengo hilo mwaka 1913. Picha| Daniel Mwingira.

Tangu wakati huo hadi sasa ghorofa hilo liko chini ya umiliki wa Wamisionari hao ambao wanalitumia kama makao makuu ya shirika hilo nchini Tanzania. 


Kwanini linaitwa  Atiman House?

Watu wengi watakuwa wanajiuliza huyo Atiman ni nani hasa mpaka shirika la Wamisionari wa Afrika wakaamua kumpa heshima hiyo ya kihistoria.

Kwa mujibu ya maandishi ya kihistoria ya Wamisionari wa Afrika katika kitabu cha ‘A History of the White Fathers in Western Tanzania’ kilichoandikwa na Padri Peter Simchile, wanamtambulisha Atimani kama Katekista Dk Andrian Atimani ambaye alikombolewa utumwani baada ya kuuzwa mara mbili akiwa na umri kati ya umri wa miaka saba na 10.

Atimani alikombolewa mwaka 1876 na Wamisionari hao waliokuwa wanatimiza malengo ya mwazilishi wao, Kardinali Lavigerie ikiwemo la kuwakomboa watumwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

Katekista Daktari  Andrian Atimani aliyekomboliwa na Wamisionari wa Afrika na jina lake likatumika kuliita ghorofa la Atiman House, miongoni majengo ya kwanza kujengwa Dar es Salaam. Picha|Africa Magazine of True Continent. 

Kilichowavutia kumkomboa na kumchukua Dk Atiman ni kwa sababu alikuwa mtumwa mwenye ufahamu mkubwa ambapo alifundishwa Ukristo na kubatizwa na Kardinali Lavigerie mwaka 1882.

Dk Atiman alipelekwa shule na baadaye kwenye chuo cha udaktari katika visiwa vya Malta ambapo alipohitimu masomo alijitolea kwenda na msafara wa saba wa wamisionari Tanganyika.

Pia alifanya kazi katika hospitali ya Shirika la Roho Mtakatifu Zanzibar. Alijifunza magonjwa ya kitropiki na aliwasili katika makazi ya ya Wamisionari ya Karema yaliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika mwaka 1889 ambapo alifanikiwa kumwoa mtoto wa Chifu wa zamani wa kabila dogo la Chata ambaye alikubali dini ya Kikristo na kubadili jina akaitwa Agnes.

Katekista Atiman na mke wake walifanikiwa kupata mtoto mwaka 1892 na kumpa jina la Joseph. Mtoto huyo baadaye alikuja kuwa  Padri wa kwanza wa jimbo la Sumbawanga pamoja na Padri Adolph mwaka 1923. 

Dkt Atiman alifariki akiwa na umri wa miaka 91 huko Karema Aprili 24,1956.

Moja picha iliyopo katika jengo la Atiman House ikionyesha kaburi la Dr Adrian Atiman baada ya kufariki. Picha| Daniel Mwingira.

 

Enable Notifications OK No thanks