Hawa ndiyo vijana 10 wenye ushawishi zaidi Tanzania

February 21, 2019 5:13 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni vijana wanaofanya vizuri katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo michezo, burudani, teknolojia, uongozi na ujasiriamali wa kijamii.
  • Wanawake watatu akiwemo Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo wamefanikiwa kuingia katika orodha hiyo.
  • Mtangazaji wa Clouds FM na mmiliki wa Ayo TV, Millard Ayo ameshika nafasi ya kwanza kama kijana mwenye ushawishi zaidi kwa mwaka 2018.
  • Ushawishi wao unatokana na mchango wanaoutoa katika kuendeleza rasilimali za Tanzania na Afrika.

Dar es Salaam. Hatimaye kampuni ya Avance Media imetoa orodha ya vijana 10 wenye ushawishi Tanzania huku Mtangazaji wa Clouds Fm, Millard Ayo akiibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza.

Ayo, ambaye ni mmiliki wa tovuti ya habari ya millardayo.com na televisheni ya mtandaoni ya Ayo TV, ameibuka mshindi wa jumla kwa kupigiwa kura nyingi akimpiku mchezaji wa soka la kulipwa wa timu ya Genk ya nchini Ubelgiji na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta aliyeshikilia nafasi hiyo ya ushawishi tangu mwaka 2017.

Samatta ambaye ameondolewa katika ushindi wa jumla, bado ameibuka mshindi katika kipengele cha michezo kama mtu mwenye ushawishi zaidi katika tasnia hiyo nchini kwa mwaka 2018.

Kampuni hiyo ya Avance Media ya nchini Nigeria imetangaza majina hayo  Februari 20, 2019 baada ya kufanya mchujo kwa vijana 50 wenye ushawishi (50 Most Influential Young Tanzanians 2018) waliobobea katika nyanja mbalimbali za maendeleo ambapo shindano hilo lilifanyika kwa kupigiwa kura mtandaoni. 

Makundi yaliyoshindaniwa katika mashindano hayo ni biashara, burudani, sheria na utawala, michezo, uongozi na uongozi wa kijamii, ujasiriamali wa kijamii na kujitolea,  mitindo na maisha. Vipengele vingine ni vyombo vya habari, sayansi na teknolojia, maendeleo binafsi na taaluma.

Licha ya Ayo kuibuka mshindi wa jumla, pia ameibuka mshindi katika kundi la bloga na mtangazaji bora. 

Wengine waliong’aa katika mashindano hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo ambaye ameshika nafasi ya kwanza katika kundi la sheria na utawala ambapo amewapiku Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Catherine Ruge; Wakili Jebra Kambole; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Zainab Katimba.

Katika kundi la maendeleo binafsi na taaluma, Badru Juma Rajab kutoka shirika la vijana la Umoja wa mataifa (YUNA) ndiye aliyeongoza na kuwabwaga washiriki wenzake ikiwemo Lameck Kiula kutoka Child in Action Foundation na Felix Manyogote (Jambo Bukoba). 

Wengine ambao wamepeperusha bendera ya vijana wenye ushawishi zaidi nchini ni pamoja na Doris Mollel kutoka taasisi ya Doris Mollel Foundation aliyeshinda kundi la uongozi na uongozi wa jamii huku Faraja Nyalandu kutoka taasisi ya Shule Direct inayowasaidia wanafunzi wa shule za sekondari kujisomea mtandaoni akiongoza katika kundi la ujasiriamali wa kijamii na kujitolea. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amechomoza katika kundi la sayansi na teknolojia huku William Mshery kutoka Vijana Think Tank akiongoza kundi la biashara.


Zinazohusiana:


Upande wa burudani, msanii wa kizazi kipya kutoka kundi la Wasafi, Diamond Platinumz ameibuka wa kwanza katika kundi hilo baada ya kuchuana vikali na wasanii wenzake, Ali Kiba, MC Pilipili,  Vanessa Mdee (V Money) na aliyewahi kuwa mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu. 

Katika taarifa iliyotolewa na Avance Media, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Prince Akpah amesema ushindi wa vijana hao sio wa kubahatisha kwa sababu ushawishi wao umekuwa ukigusa maisha ya watu na kazi na vipaji vyao vimesaidia kuleta mabadiliko chanya ikiwemo kutengeneza ajira kwa vijana wengine nchini Tanzania na Afrika. 

Mashindano mengine ya kuwatafuta vijana wenye ushawishi zaidi Tanzania yatafanyika tena mwaka huu, ambapo ni fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao katika kutatua changamoto za jamii na kutambulika kimataifa.

Enable Notifications OK No thanks