Fanya haya kuepuka uvivu kazini

March 12, 2019 6:11 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kama uvivu utapewa nafasi kubwa katika shughuli za kikazi na biashara unajenga tabia ambayo ikiota mizizi inaathiri kabisa maisha yako.
  • Ongeza ubunifu, kamilisha kazi kwa wakati na jichanganye na marafiki wachapa kazi wenye malengo.
  • Jenga tabia ya kufanya mazoezi kila siku ili kuchangamsha akili na uwezo wa kiutendaji.

Juhudi na maarifa ni njia mojawapo ya kufanikiwa katika kila jambo unalofanya, iwe ni biashara au kazi. Lakini kuna wakati tunajikuta katika hali ya kuchoka na kushindwa kufanya yale tunayotarajia yatokee. 

Hali hiyo hutafsiriwa kama uvivu wa kutokufanya kazi fulani kwa muda fulani ambapo husababisha mipango iliyopangwa isifanyike kwa wakati au isifanyike kabisa. 

Kama uvivu utapewa nafasi kubwa katika shughuli za kikazi na biashara unajenga tabia ambayo ikiota mizizi inaathiri kabisa maisha ya mtu. Huenda na umekuwa ukijiuliza kwanini mambo yako hayaendi, huenda una ugonjwa wa uvivu. Sasa ufanye nini kuepuka uvivu: 

 

Ongeza ubunifu 

Mfanikio ya kibiashara au kazi hutegemea zaidi uwezo wako wa kubuni mambo mapya ili kuboresha utendaji kazi wa kila siku na kuongeza tija. Epuka mambo yale yale kila siku, akili inachoka na kuzoea. 

Ichangamshe akili kwa kufanya tofauti na ulivyozoea ili kuiamsha kutafuta namna ya kuendana na mabadiliko katika maisha yako ambapo itakuongezea nguvu ya kufanya kazi kwa juhusi na maarifa. 

Mwandishi Sierra Pedraja katika moja ya makala zake anasema,”Unatakiwa kufanya kazi kwa bidii kuacha alama.”


Soma zaidi: Jinsi unavyoweza kuepuka sonona isiharibu maisha binafsi, kazi 


Kamilisha kazi kwa wakati

Acha tabia ya kuairisha kazi uliyoanza kuifanya (procrastination). Kama utaendelea kuairisha ukidhani una muda mwingi wa kuifanya, utajikuta unaingiwa na uvivu na matokeo yake itajengeka tabia ndani yako ya kushindwa kukamilisha kazi kila unapoanza. 

Dk Marty Nemko katika jarida la Phychology Today anaeleza kuwa ili mtu aondokane na kuahirisha mambo ni lazima atumie muda wake vizuri na kuigawanya kazi katika vipengele ili kufahamu itatumia muda gani kuikamilisha.

Wachunguze marafiki zako

Marafiki wana nafasi kubwa ya kukukwamisha au kufanikisha katika maisha. Chagua marafiki wachapa kazi ambao wakati wote watakuhimiza kufanya kazi na kutekeleza mipango yako. 

Tengeneza mtandao wa marafiki wanaopenda kujifunza hii itakusaidia sana pindi utakapokuwa unatumia muda nao kwa sababu utaona namna wanafanya kazi kwa kujituma utavutiwa nawe utahamasika na kuacha uvivu.

Uvivu ukiachwa kwa muda mrefu unajenga tabia inayoweza kuwa na matokeo hasi katika shughuli za kila siku za kazi. Picha| CareerAddict

Weka malengo ya maisha

Acha kuishi bila mpangilio. Fahamu hakika nini kusudi la maisha yako, weka vipaumbele na wekeza muda na nguvu zako katika kutekeleza. 

Kukosa malengo ama uelekeo wa maisha ni njia mojawapo ya kukaribisha uvivu ambao utakukudimiza kabisa. 

Usiishie tu kujiwekea malengo lakini bali panga namna ya kuyatekeleza kwa awamu kwa kujikumbusha mara kwa mara. Hii itakuwasaidia kukuondolea uvivu katika mwili wako.

Pale unapokuwa na malengo katika maisha huwezi kuwa mvivu utakuwa unajituma kuhakikisha unafanikisha malengo yako hayo. Lakini pia hakikisha unajikumbusha malengo yako siku ili upate nguvu ya kuyafanya na usijisahau. 

 

Jenga mazoea ya kufanya mazoezi 

Kuna wakati unakuwa unahisi kuchoka katika kazi unayofanya.Kama uko ofisini, simama na fanya mazoezi ya kujinyoosha au toka nje ya ofisi pata upepo kidogo alafu rudi ndani hii itakupa nguvu nyingine na ari ya kufanya kazi yako. 

Kama uko nyumbani, punguza kukaa muda mrefu na kuangalia televisheni badala yake fanya matembezi ili kupata hali tofauti na uliyozoea nyumbani. Hii itakusaidia kujifunza vitu vingi njiani ikiwemo kukutana na watu wapya wenye mawazo chanya.

Mazoezi ni njia mojawapo ya kuwa na msawazo mzuri wa akili. Tumiamuda wa mapumziko ukiwa kazini kutembea, kujinyoosha na hata kubadilisha mikao ili kuondoa uchovu mwilini. Picha|Greatist.

Enable Notifications OK No thanks