Mkaa, kuni vyachangia kupaa mfumuko wa bei
Miongoni mwa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kwa kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei katika kipindi hicho ni zile za nishati zikiwemo kuni kwa asilimia 27.2, mkaa (asilimia 13.1), dizeli (asilimia 8.3) na mafuta ya taa kwa asilimia nane. Picha|Mtandao.
- Taarifa ya NBS yaeleza mfumuko wa bei wa Taifa umeongezeka kidogo katika mwaka ulioshia Machi 2019 hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3 ya Februari mwaka huu.
- Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Machi 2019 umepungua mara tano hadi asilimia 0.1 kutoka asilimia 0.5 iliyorekodiwa katika mwaka ulioshia Februari 2019.
Dar es Salaam. Mfumuko wa bei wa Taifa umeongezeka kidogo katika mwaka ulioshia Machi 2019 hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3 iliyorekodiwa Februari mwaka huu hali hiyo ikichangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
“Hii inaamanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka Machi 2019 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Februari 2019,” inasomeka sehemu ya taarifa ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Aprili 8, 2019).
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mfumuko huo wa bei unatokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Machi 2019 ikilinganishwa na kile kilichoishia Machi 2018.
Zinazohusiana: Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Januari
Miongoni mwa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kwa kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei katika kipindi hicho ni zile za nishati zikiwemo kuni kwa asilimia 27.2, mkaa (asilimia 13.1), dizeli (asilimia 8.3) na mafuta ya taa kwa asilimia nane.
Bidhaa nyingine zilizochangia mfumuko huo wa bei ni mavazi na viatu kwa asilimia 3.4, kodi ya pango (asilimia 4.7), malazi kwenye hoteli (asilimia 5.7) na chakula na vinywaji kwenye migahawa kwa asilimia 4.6.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Machi 2019 umepungua mara tano hadi asilimia 0.1 kutoka asilimia 0.5 iliyorekodiwa katika mwaka ulioishia Februari 2019.