Rais Magufuli aiongezea muda Bodi iliyowahi ‘kuvunjwa’ na Kigwangalla
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye yeye na wajumbe sita wameongezewa muda wa kufanya kazi hadi Aprili 23, 2022. Picha|Mtandao.
- Rais John Magufuli ameongeza muda wa miaka mitatu kwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliyokuwa imalize muda leo (Aprili, 2019).
- iliwahi kuvunjwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla Januari 18, 2019 lakini mwenyekiti wake alipinga uamuzi wa waziri.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameongeza muda wa miaka mitatu kwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliyokuwa imalize muda leo (Aprili, 2019).
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ameeleza kuwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa bodi hiyo wameongezewa muda hadi Aprili 23, 2022.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Bodi hiyo inaongozwa na Mwenyekiti, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na wajumbe sita ambao ni Augustine Kungu Olal, Zabein Muhaji Mhita na Richard Rugimbana. Wengine ni Mark Leveri, Ally Hussein Laay na Ibrahim Mussa.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Ikumbukwe kuwa bodi hiyo iliyoongezewa muda wake iliwahi kuvunjwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla Januari 18, 2019 kwa kile alichodai kuwa imeshindwa kutekeleza maagizo ya wizara kwa wakati ikiwemo kuweka mabango yanayotangaza utalii katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam na katika eneo la ofisi za bodi hiyo na kuweka majarida ya utalii katika ndege za Tanzania.
Hata hivyo, siku mbili baada ya Kigwangalla kuvunja Bodi hiyo, Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Mihayo alipinga uamuzi huo na kusema Bodi inatimiza majukumu yake kikamilifu na kulikuwa hakuna ulazima wa waziri kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo.
“Hiyo ina maana kwamba kisheria waziri hana mamlaka ya kuvunja bodi kwa maana unapoivunja bodi kila kitu kinatoweka, lakini kama sehemu inabaki, hujaivunja bodi ndiyo maani mimi bado ni mwenyekiti wa bodi ambaye hata hivyo sina wajumbe,” alinukuliwa Jaji Mihayo na Wanahabari Januari 21, 2019.