WhatsApp yatoa mbinu za kujikinga na shambulio la udukuzi linalowakabili
Ili kukabiliana na uvamizi huo, WhatsApp yenye watumiaji zaidi ya bilioni 1.5 duniani haraka iliwataka wote wanaotumia programu hiyo kuiboresha katika toleo jipya ili waweze kuepuka kudukuliwa. Picha|Mtandao.
- Kampuni hiyo inayomilikiwa na Facebook imetaka watumiaji wote zaidi ya bilioni 1.5 kuboresha programu katika toleo la sasa kuepuka uvamizi wa kimtandao wa hivi karibuni.
- Wadukuzi wanadaiwa kuwa walilenga kunyonya taarifa za faragha za watumiaji wa mtandao huo hasa wanaharakati na wahabari.
Dar es Salaam. Iwapo unatumia mtandao wa WhatsApp utalazimika kuboresha programu hiyo kwenye kifaa chako ili kuimarisha mfumo wa usalama baada ya kutokea uvamizi uliolenga kunyonya taarifa za watumiaji wa mtandao huo.
Imeelezwa kuwa uvamizi huo ulifanywa na wadukuzi waliotumia programu inayodaiwa kurandana na ile inayotengenezwa na kampuni ya teknolojia ya Israel (NSO) inayofahamika kwa kutengeneza mifumo ya udukuzi kwa ajili ya Serikali.
Katika uvamizi huo, wadukuzi waliingilia mfumo wa simu wa mtandao huo maarufu wa kuchati ili kuweza kudukua taarifa za watumiaji wa simu zinazotumia programu endeshi za Android na iOS hususan wanaharakati na wanahabari.
NSO imekana kuhusika katika shambulio hilo la kimtandao katika siku hizi za karibuni.
Zinazohusiana: WhatsApp inavyowabeba wajasiriamali Tanzania
Shirika la habari la The New York Times la Marekani limeeleza kuwa wahandisi wa WhatsApp walikesha siku nzima ya Jumatatu katika kukabiliana na uvamizi huo uliokuwa ukihatarisha kuyeyuka kwa faragha ya watumiaji wa mtandao huo unaomilikiwa na Facebook ya Marekani.
Ili kukabiliana na uvamizi huo, WhatsApp yenye watumiaji zaidi ya bilioni 1.5 duniani haraka iliwataka wote wanaotumia programu hiyo kuiboresha katika toleo jipya ili waweze kuepuka kudukuliwa.
“WhatsApp inawasisitizia watu wote kuboresha programu zao katika toleo la sasa na kuhakikisha kuwa programu zao endeshi zimeboreshwa kila wakati ili kujilinda na uvamizi wa taarifa ambazo zimehifadhiwa katika simu zao za mkononi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya WhatsApp kwa umma.