Rais Magufuli aelekea Afrika Kusini, Namibia
- Katika safari hiyo, Dr Magufuli atahudhuria uapisho wa rais mteule wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kabla ya kuelekea Namibia kwa ajili ya ziara rasmi ya kitaifa.
- Hii ni zaira ya pili kufanywa ndani ya mwezi mmoja na Rais Magufuli baada ya kuzuru Malawi mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameondoka nchini kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa ikiwa ni moja safari chache alizozifanya kiongozi huyo wa nchi tangu aingie madarakani miaka mitatu na nusu iliyopita.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo (Mei 24, 2019) inaeleza kuwa baada ya kuhudhuria sherehe hizo, Rais Magufuli ataelekea Namibia katika ziara rasmi ya kitaifa ambako atazindua barabara iliyopewa jina la Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
“Katika safari hiyo Rais Magufuli ameongozana na Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Philip Mangula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Ujumbe huo wa Rais Magufuli umeondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Kikwete na Mangula wamesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina, “uhusiano mkubwa na wa kihistoria na kwamba Serikali na chama zina kila sababu ya kudumisha uhusiano na ushirikiano huo.”
Profesa Kabudi amesema Rais Magufuli atazindua mtaa huo wa Mwalimu Nyerere kutokana na kutambua mchango alioutoa Baba wa Taifa katika ukombozi wa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.
Safari hiyo ya Rais Magufuli ni ya pili kufanywa ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzuru Malawi mwishoni mwa Aprili mwaka huu ambapo pamoja na mengine alifungua msimu wa soko la tumbaku.
Rais Dkt. @MagufuliJP aelekea Afrika Kusini kuhudhuria Sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Nchi hiyo Mhe. Cyril Ramaphosa pic.twitter.com/MIsN1BJiI9
— Msemaji Mkuu wa Serikali (@TZMsemajiMkuu) May 24, 2019