Google Maps yaja kivingine, watumiaji wake kufahamishwa kasi wanayotumia barabarani
- Imeongeza kipengele cha kupima kasi ya mwendo anayotumia mtu wakati akiendesha gari (Speedometer).
- Inasaidia kuepusha ajali na makosa wakati ukitumia barabara.
Dar es Salaam. Watumiaji wa huduma ya programu tumishi (App) ya Google Maps sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kufanyiwa maboresho yanayowezesha watumiaji hao kufahamu kasi ya mwendo wanaotumia katika safari zao.
App hiyo inayomilikiwa na kampuni ya teknolojia ya Google ya nchini Marekani, imeongezewa kipengele cha mita ya kupima kasi (Speedometer) inayoonyesha mwendo anaotumia mtu wakati akikatiza mitaa mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Google iliyotolewa hivi karibuni, licha ya ukweli kuwa magari yana ‘dashboard’ inayopima kasi ya gari, bado watu wanahitaji huduma hiyo kwenye simu zao wakati wakitumia Google Map.
Sababu kubwa ni kuwa inakurahisishia kufahamu kasi kwa haraka wakati ukiangalia mahali unapokwenda bila kurudi tena kwenye dashboard ya gari yako, jambo linalookoa muda na kukufanya uwe makini barabarani. Hii pia inasaidia kupunguza hatari ya kupata ajali.
Soma zaidi:
Unaweza kupata kipengele hicho kipya katika mapendekezo ya programu chini ya mipangilio ya ufuatiliaji (Navigation Settings) ambapo itaonyesha ‘speedometer’ upande wa chini kushoto wakati ukitumia mwongozo wa kuendesha gari.
Hata hivyo, huduma hiyo haijaanza kuonekana kwa watumiaji wote duniani kwa sababu bado inaboreshwa zaidi ili ikiachiliwa ilete matokeo yaliyotarajiwa.
Inaelezwa kuwa sasa inapatikana katika nchi za Argentina, Australia, Ubelgiji, Brazil, Canada, Jamhuri ya Czech,, Finland, Ujerumani, India, Uholanzi, Poland, Sweden, Taiwan, Uingereza, na Marekani.
Muonekano mpya wa Google Maps ukiwa na kipengele kinachoonyesha ‘Speedometer’ inayowasaidia watumiaji kujua kasi ya mwendo wanapokuwa barabarani. Picha|Mtandao.