Waziri Kabudi aeleza ‘walivyotoana jasho’ na kampuni ya Bharti Airtel kupata Sh1 bilioni kila mwezi

June 11, 2019 9:05 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema wawakilishi wa kampuni hiyo walikuwa hawayumbishwi na walisimamia walichokiamini. 
  • Bado hawajakamilisha baadhi ya maridhiano ambayo yanamuhitaji Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 
  • Pamoja na msuguano huo, Serikali imeongeza hisa katika kampuni ya Airtel Tanzania na kupata malipo maalum ya Sh1 bilioni kila mwezi kwa miezi 60 ijayo.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza jinsi kamati aliyoiongoza ‘ilivyotoana jasho’ na kampuni ya Bharti Airtel katika kutafuta maridhiano ya umiliki wa Airtel Tanzania yakiwemo ya kutoa malipo maalum ya Sh1 bilioni kila mwezi kwa miezi 60 kwa Serikali.

Januari 10, 2018, Rais John Magufuli uliteua kamati iliyoongozwa na Prof Kabudi iliyokuwa inafanya ufuatiliaji wa umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel Tanzania inayomilikiwa na Bharti Airtel ya nchini India. 

Kwa mujibu Prof Kabudi kamati hiyo ilifanya majadiliano na Bharti Airtel kwa awamu tano na mnamo Januari mwaka huu, mkataba wa makubaliano ulisainiwa na kuipa Serikali baadhi ya mafanikio ikiwemo kuongeza umiliki wa hisa za Serikali ndani ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 bila kulipia.

Makubaliano mengine ni kubadilisha muundo wa bodi na menejimenti ya Airtel Tanzania ambapo Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu yaani CEO sasa wanateuliwa na Serikali. 

“Airtel Tanzania imekubali kulipa kiasi cha Sh1 bilioni kila mwezi kama malipo maalum kwa Serikali kwa muda wa miaka mitano ijayo kuanzia mwezi wa nne mwaka huu na Sh3 bilioni zilizotolewa leo ni sehemu ya malipo hayo kwa mwezi Aprili, Mei na Juni,” amesema Prof Kabudi. 

Waziri huyo amesema Bharti Airtel imefuta deni na madai mengine ya kampuni ya Airtel kiasi cha Dola za Marekani zaidi 407.38 milioni (sawa na Sh937 bilioni) jambo lililoipunguzia mzigo Serikali kulipa deni la Sh 459.13 bilioni kama mwanahisa. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, Waziri Kabudi amesema haikuwa rahisi kufikia maridhiano hayo na walilazimika ‘kutoana jasho’ na wawakilishi wa Bharti Airtel ambao walikuwa wamejipanga vizuri kutetea hoja zao dhidi ya Serikali. 

Amesema timu ya Bharti Airtel ilioongozwa na Mshauri Mkuu wa kampuni hiyo, Mukesh Bhavnani ambaye alisimama kidete kutetea maslahi ya kampuni yake na hakukubali kuyumbishwa kabisa na timu ya Tanzania. 

“Huyu Mukesh akipewa maelekezo na Sunil Mittal habadili hata sentensi, niseme leo kwa sababu ni siku ya shangwe, kundi zima hili tulimchukia Mukesh mpaka baadaye tulipojua kumbe huyu ni mtumishi mwaminifu wa Bharti.

“Yaani atakuja hapa Mhe. Rais, tumefanya kikao humu ndani anatoka nje no! (Hapana) Baadaye tukajua kumbe ni maagizo ya Bharti tukasema tuige mfano wake, tukipewa maagizo hakuna kubadili mstari,” alisema Prof Kabudi jana wakati wakipokea maalipo maalum ya Sh3 bilioni ya miezi mitatu iliyopita kutoka Bharti Airtel. 

Amesema kutokana na umahiri wa Mukesh wa kutetea hoja, bado hawajafikia muafaka katika baadhi ya mambo ambayo anahitajika kuwepo Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil Mittal  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kukamilisha maridhiano hayo yaliyoanza mwaka jana. 

“Na hata leo, Mhe. Rais tulikuwa na wakati mgumu Mukesh toka Jumanne yuko hapa amekataa katakata, leo ndiyo tumeyaongea na ndugu yangu Bwana Sunil Mittal na tutayarekebisha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesisitiza Waziri huyo.  

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Sh3 bilioni kama malipo maalum kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Bharti Airtel Sumil Bharti Mittal (kushoto), jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kampuni hiyo kufikia muafaka na Serikali juu ya umiliki wa Airtel Tanzania. Picha|Mtandao.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameitaka kamati ya maridhiano kuhakikisha wanamaliza haraka mambo ambayo bado hawajafikia muafaka ili shughuli zingine ziendelee.  

Timu ya Tanzania iliyokua ikichuana na wawakilishi wa Bharti Airtel ailikuwa na wajumbe mahiri kutoka taasisi za Serikali wakiwemo; Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Jim Yonazi; na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya simu Tanzania (TTCL), Dk Omary Nundu.

Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba; Mchumi Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Nuru Ndile; Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Pius Nyagoga na  Aziz Dachi. 

Prof Kabudi amesema hayo ni mafanikio makubwa kwa sababu Serikali haijawahi kupata gawio lolote kutoka Airtel kwa takriban miaka 10 iliyopita licha ya kuwa na hisa katika kampuni hiyo ya simu yenye watumiaji takribani 10.9 milioni hadi Desemba 2018, ikishika nafasi ya tatu baada ya Vodacom na Tigo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Mwenyekiti Mtendaji wa Bharti Airtel Sumil Bharti Mittal amesema mchakato wa kufikia maridhiano ulianza ukiwa mgumu huku jambo lililomsumbua zaidi ni msimamo wa Serikali kuwa ubinafsishwaji Airtel Tanzania haukufuata taratibu zinazotakiwa.

“Kampuni hii (Airtel Tanzania) imekuwa ikipata hasara wakati wote hivyo sehemu kubwa ya fedha imekuwa ikitumika kukabiliana na hasara hiyo. Hata hivyo, tumepata namna bora angalau ya kulipa kitu fulani,” amesema Mittal huku akipongeza maridhiano hayo kuanza yanaanzisha safari mpya ya kampuni hiyo ya mawasiliano.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV