Dk Mpango – Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania

June 13, 2019 7:28 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema wastani wa pato la kila mtu uliongezeka na kufikia Sh2.46 milioni mwaka 2018 kutoka Sh2.32 milioni mwaka 2017.
  • Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ni Sanaa na burudani, ujenzi, shughuli za kitaaluma huku kilimo kikikua kwa asilimia 5.3. 

Dar es Salaam. Serikali imesema kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2018 iliongezeka hadi asilimia 7 kutoka asilimia 6.8 iliyorekodiwa mwaka 2017 huku wastani wa kipato cha mtu ndani mwaka huo mmoja kikiongezeka kwa zaidi ya Sh130,000.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ameliambia Bunge leo wakati akiwasilisha hotuba ya hali ya uchumi mwaka 2018 na Mpango wa Serikali wa 2019/20 kuwa uchumi ulikuwa kwa asilimia saba 2018 kutoka asilimia 6.8 kwa bei za kizio cha mwaka 2015.

Ukuaji huo, kwa mujibu wa Dk Mpango ulichagizwa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika ujenzi wa reli, viwanja vya ndege, kutengemaa kwa upatikanaji wa umeme, kuimarika kwa huduma za usafirishaji na hali ya hewa iliyowezesha upatikanaji mzuri wa chakula na mazao yasiyo ya chakula.

Amesema shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi zaidi mwaka 2018 ni sanaa na burudani kwa asilimia 13.7, ujenzi (asilimia 12.9), uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (asilimia 11.8%), shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi (asilimia 9.9), habari na mawasiliano (asilimia 9.1) na kilimo kilikua kwa kasi ya asilimia 5.3.

“Sekta zilizotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ni kilimo asilimia 28.2, ujenzi (asilimia 13), na biashara na matengenezo kwa asilimia 9.1,” amesema Dk Mpango.

Wakati baadhi ya watu wakisema upatikanaji wa fedha umekuwa mgumu kwa sasa, Dk Mpango ameliambia Bunge kuwa wastani wa pato la kila mtu liliongezeka kwa zaidi ya Sh130,000 ndani ya mwaka mmoja.

“Wastani wa pato la mtu kwa mwaka 2018 liliongezeka hadi Sh2,458,496 kutoka Sh2,327,393 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 5.6. Kiwango hicho cha wastani wa pato la kila mtu ni sawa na Dola za Marekani 1,090 mwaka 2018 kutoka Dola za Marekani 1,044 juu zaidi kwa asilimia 4.4,” amesema Dk Mpango leo (Juni 13, 2019).

Enable Notifications OK No thanks