Rwanda yazifuata Kenya, Tanzania kutoa pasipoti za kielektroniki

June 29, 2019 9:50 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Inakua nchi ya nne katika jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa pasipoti hizo kwa raia wake.
  • Pasipoti hiyo itarahisisha safari na biashara ya mipakani katika jumuiya hiyo.

Hatimaye Rwanda imeanza kutoa pasipoti ya kielektroniki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa raia wake ikiwa ni hatua ya kurahisisha na kuongeza wigo wa safari na biashara ya mipakani miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 

Rwanda inakuwa nchi ya nne katika jumuiya hiyo kutoa pasipoti za kielektroniki  ikiungana na nchi za Kenya, Tanzania na Uganda ambazo tayari zinatoa pasipoti hizo kwa raia wake.  

Uzinduzi wa pasipoti za kielektroniki katika nchi ya Rwanda umefanyika jana (Juni 29, 2019) jijini Kigali na Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji wa nchi hiyo, Francois Regis Gatarayiha. 

Akizungumza na vyombo habari, amesema pasipoti hiyo ya Afrika Mashariki itachagiza biashara na usafiri wa mipakani na kuimarisha ushirikiano wa jumuiya hiyo. 

Pasipoti hiyo imeunganishwa na ‘chip’ ndogo ya kielektroniki ambayo ina taarifa muhimu za mmiliki ikiwemo jina, mwaka wa kuzaliwa na taarifa nyingine za makazi. 

Gatarayiha amesema pasipoti hiyo imezingatia maelekezo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na kuifanya pasipoti hiyo kukubalika duniani. 


Soma zaidi: 


Uamuzi wa kutumia pasipoti za kielektroniki zinazofanana ulifikiwa katika kikao cha 17 cha wakuu wa nchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Machi 2016 jijini Arusha. 

Pasipoti za kielektroniki zinatajwa kuwa ni salama zaidi kuzitumia kwa sababu zimeunganishwa na mifumo ya usalama mtandaoni, jambo linalofanya iwe vigumu kwa mtu kuiba au kughushi taarifa za mtumiaji zilizopo katika kanzi data (data base).

Lakini ni fursa kwa wananchi wa Afrika Mashariki hasa katika biashara inayofanyika mipakani na inarahisisha utambuzi wa raia kwa haraka katika vituo vya uhamiaji vilivyopo kwenye viwanja vya ndege na mipakani.

Hata hivyo, pasipoti hizo mpya ambazo zinachukua nafasi ya zile za zamani zinawahakikishia wananchi wa Afrika Mashariki kuishi na kufanya kazi katika nchi wanachama bila vikwazo. 

Enable Notifications OK No thanks