Wafahamu tausi ambao Magufuli alimzawadia Rais Kenyatta

July 8, 2019 7:41 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hupatikana katika makazi ya viongozi mbalimbali duniani.
  • Hutumika kama mapambo na kivutio cha wageni.
  • Baadhi ya nchi humtumia tausi katika shughuli za kidini na utamaduni. 

Dar es Salaam. Mwishoni mwa wiki, Rais wa Tanzania, John Magufuli alimzawadia jirani yake wa Kenya, Rais Uhuru Kenyatta ndege wanne aina ya tausi kama kumbukumbu ya uhusiano, urafiki na ujirani mwema kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.

Lakini umewahi kujiuliza tausi wanavyozaliana, mazingira wanayoishi, sifa walizonazo na kwanini wanapatikana katika makazi mbalimbali ya viongozi duniani? www.nukta.co.tz tunakuletea undani wa ndege huyo ambaye ana sifa za kipekee.

Rais Magufuli alitoa zawadi hiyo Julai 6, 2019 katika makazi yake yaliyopo katika kijiji cha Mlimani , Wilaya ya Chato mkoani Geita alipokutana na Kenyatta wakati wa mapumziko.  

Zawadi ya kipekee kwa Kenyatta

“Nimeguswa, sijawahi kugawa tausi kwenye nchi yoyote kwa sababu wana historia ya nchi yetu. Kwa heshima kubwa na mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya, nimekubali na hili nataka kulisema wazi.

“Najua watu wataandika lakini hili limenigusa kutoka moyoni, nitatoa tausi wanne watapelekwa Kenya kwa Kenyatta,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa baada ya miaka kadhaa ndege hao watazaliana na kurejeshwa tena Tanzania.

Wapo tausi wanaofugwa na wale wanaoishi porini. Wote kwa pamoja ni mapambo na kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea maeneo waliyopo. Picha|Mtandao.

Tausi wamekuwa wakitumika kama mapambo na kivutio kwa wageni hasa wanaotembelea katika Ikulu za nchi mbalimbali duniani kutokana na umahiri wake wa kuinua na kuchanua mkia wake na kutoa milio yenye ishara mbalimbali. 

Kwa kawaida tausi wana rangi ya bluu na kijani japo tausi weupe wapo pia.  Urefu wake ni sentimita 200 hadi 300 kwa tausi dume huku mkia wake ukiwa na urefu wa sentimita 150 hadi 170. 

Tausi jike ana urefu wa sentimita 150 hadi 250 kutegemea na eneo alilopo na ulinzi wake. Tausi wanaweza kuishi mpaka miaka 20 ikiwa watakuwa mahala salama na kutunzwa vizuri. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Sciencing inayohusika na sayansi mbalimbali ikiwemo ya ndege, tausi wakichanua mkia wake au kutoa mlio, basi kuna jambo linafanyika ikiwa ni njia ya kuwasiliana baina yao. 

Mkia wenye ujumbe

Inaeleza kuwa tausi dume ndiye anayechanua mkia wake na siyo jike, ikiwa ni ishara kuwa unamhitaji jike ili washiriki tendo la kujamiana kwa sababu majike yanavutiwa na dume lenye mkia mkubwa na mzuri. 

Ili kuonyesha jike limefurahishwa na dume lililojichanua, hupiga kelele ambazo huwa ni milio inayovutia kwa binadamu. 


 Zinazohusiana:


Lakini tausi wana kitu cha tofauti kwa sababu rangi yake ndiyo huwa rangi ya macho yao, jambo linalowafanya kupendezesha mazingira waliyopo. Chakula chao ni mijusi, nyoka wadogo, mbegu za nafaka na mizizi laini.

Tausi jike hutaga yai moja hadi manane ambapo huatamia kati ya siku 21 hadi 35 kutegemea na hali ya hewa.

Kwa mujibu wa kampuni ya utalii ya Mark International Tour and Travel, tausi jike hukaa na watoto wake kwa karibu miezi sita na inapofika miezi nane tayari huwaacha ili waanze kujitegemea. 

Madume huanza kupanda yakiwa na umri wa miaka minne na majike huanza kupandwa wakiwa na miaka mitatu na nusu.

 Huko India ni zaidi ya ndege

Nchini India wanamtumia tausi kama ndege wa Taifa kwa sababu ya umuhimu wake katika shughuli za kidini na kitamaduni na hivyo kupewa heshima kubwa na wananchi. 

Hata hivyo, wapo tausi wanaofugwa na wale wanaoishi porini. Wote kwa pamoja ni mapambo na kivutio kikubwa kwa wageni wanaotembelea maeneo waliyopo. 

Enable Notifications OK No thanks