Tunayoyafahamu kuhusu Kisimiri, shule iliyoongoza kitaifa kidato cha sita

July 11, 2019 4:33 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Haijawahi kutoka katika orodha ya shule 10 bora kitaifa kwa miaka nane mfululizo.
  • Ina michepuo miwili tu ya PCM na HKL ambayo wanafunzi hufaulu vyema. 
  • Ilijengwa mwaka 2002 kwa nguvu za wananchi.
  • Mwaka huu wanafunzi 58 kati ya 60 wamepata daraja la kwanza huku wawili wakipata daraja la pili. 

Dar es Salaam. Habari ya mjini leo kama wasemavyo vijana, ni matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2019 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta). 

Macho na masikio yapo zaidi kwa Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyoongoza kitaifa katika matokeo hayo. 

Shule hiyo, inayomilikiwa na Serikali iko mkoani Arusha, imefanikiwa kuzipita shule kongwe na zile za binafsi ambazo zimekuwa na historia nzuri ya ufaulu katika ngazi hiyo ya elimu. 

Katika matokeo ya mwaka huu, Kisimiri ambayo ilikuwa na watahiniwa 60 imeonyesha cheche zake baada ya wanafunzi 58 kupata daraja la kwanza huku wawili waliobaki wakipata daraja la pili. 

Kwa matokeo hayo, ni sawa na kusema asilimia 96.6 ya wanafunzi wake wamepata daraja la kwanza. Hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la tatu hadi sifuri (III-0). 

Ufaulu wa Kisimiri siyo wa kubahatisha

Mafanikio ya shule hiyo ya mchanganyiko yaani wavulana na wanasichana, siyo ya kubahatisha, kwani imekuwa ikifanya vizuri tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hasa katika mpangilio wa madaraja ya ufaulu. 

Uchambuzi wa matokeo ya Necta uliofanywa na www.nukta.co.tz katika kipindi cha miaka nane iliyopita (2012-2019) umebaini kuwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita katika kipindi hicho ni 466 ambapo ni mwanafunzi mmoja tu ndiye aliyewahi kupata daraja la nne mwaka 2012.

Daraja sifuri wanafunzi hao husikia tu kwa majirani zao kwa kuwa hakuna hata mwanafunzi mmoja katika kipindi hicho aliwahi kupata daraja la kwanza ndiyo limekuwa na wanafunzi wengi zaidi wanaofikia 313, daraja la pili ni 117 huku daraja la tatu wakiwa ni 35 tu. 

Lakini mwaka 2016, 2018 na mwaka huu, shule hiyo haikuwa na  wanafunzi waliopata daraja la III, IV wala 0. 

Bado inatamba 10 bora kitaifa

Hata katika mpangilio wa ufaulu wa shule kitaifa, bado Kisimiri inachuana vikali na shule kongwe na za binafsi kuhakikisha haitoki katika kundi hilo la dhahabu. 

Kisimiri ambayo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi haijawahi kutoka kwenye kundi la shule 10 bora kitaifa tangu mwaka 2012 ambapo ilishika nafasi ya tatu kitaifa.

Mathalani, mwaka 2018 katika matokeo ya kidato cha sita ilikuwa shule ya pili kitaifa chini kidogo ya Kibaha ambayo ilishika nafasi ya kwanza. Mwaka 2016 haikufanya makosa hata kidogo ikafanikiwa kupanda kileleni hadi kuwa shule ya kwanza Tanzania kwa ufaulu mzuri.

Licha ya kuwa katika nafasi nzuri kitaifa katika miaka nane iliyopita, imeendelea kuonyesha ubabe wake hata katika ngazi ya mkoa kwa kuzikimbiza shule za Arusha. 

Katika kipindi chote cha miaka nane imekuwa ikishika nafasi ya kwanza isipokuwa mwaka 2013 ambapo ilishika nafasi ya pili ikiwa nyuma ya shule ya Sekondari ya Ilboru. 

Jengo la shule ya Kisimiri iliyopo mkoani Arusha. Ilijengwa mwaka 2002 kwa nguvu za wananchi. Picha|Mtandao.

Idadi ya wanafunzi, michepuo yaibeba 

KisimiriHuenda mafanikio ya Kisimiri kwa upande mwingine yakawa yanachangiwa na idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kidato cha tano kila mwaka.

Uchambuzi wa www.nukta.co.tz umebaini kuwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita kila mwaka katika kipindi cha miaka nane iliyoyopita haijawahi kuvuka wanafunzi 67. 

Idadi ya juu kabisa ya wanafunzi wengi waliohitimu katika shule ilikuwa mwaka jana ambapo walikuwa 67 na idadi ya chini kabisa ilikuwa mwaka 2013 ambapo walikuwa wanafunzi 50. 

Kwa muktadha huo, shule hiyo ina uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi, jambo linalowafanya walimu kuwafikia wanafunzi wote kwa urahisi na kuwapatia maarifa yanahitajika kujibu mtihani. 

Kama hiyo haitoshi, tofauti na shule zingine, Kisimiri ina michepeo miwili tu ya PCM (Masomo ya Fizikia, Kemia na Advanced Mathematics) na HKL (Historia, Kiswahili na Language). 

Walijatabiria ushindi hata kabla ya kufanya mitihani

Mwalimu Mkuu wa shule ya Kisimiri, Valentine Tarimo hivi karibuni aliiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kufanya vizuri kwa shule hiyo ya sio uchawi bali ni jitihada za pamoja kati ya wanafunzi na walimu.

“Ufaulu wetu unachagiwa na ushirikiano mkubwa ulipo kati ya walimu na wanafunzi kwa kufanya kazi kwa bidii bila kupoteza muda kama Mheshimiwa Rais Magufuli anavyosema hapa kazi tu sisi tunatasfri kwa vitendo,”alisema Tarimo.

Amesema kuwa kila mwaka, darasa linalotaka kuweka historia yake yenyewe ama kuongoza kishule au ufaulu wa madaraja hivyo kufanya kila mwanafunzi wa kila darasa kuweka jitihada zake binafsi sambamba na hilo darasa.

“Ni kama vita kila mtu anajiandaa kupambana  na sisi tumejianda vizuri kama shule nyingine zote tunatumani kufanya vizuri lakini tusuburi matokeo yatakabotolewa na Necta yatakuaje,” alisema Mkuu huyo wa shule ya Kisimiri kabla ya kuanza mitihani kidato cha sita Mei, 2019. 

Ripoti hii imeandikwa na Daniel Samson na Daniel Mwingira.

Enable Notifications OK No thanks