Nukta Africa yateuliwa kuingia katika programu ya uwekezaji ya Seedstars

July 17, 2019 2:57 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Startups za Tanzania zilizochaguliwa ni KilimoGuide, FixChap, Peter’s Daughter, Kasome International na Nukta. Picha|Mtandao.


  • Programu hiyo inalenga kuzijengea uwezo na kuziimarisha kampuni zinazochipukia (startups) kujiendesha kibiashara.
  • Nukta Africa ni miongoni mwa kampuni 40 za Afrika ambazo zimeingia katika awamu ya kwanza ya programu hiyo. 

Dar es Salaam. Kampuni ya Nukta Africa imekuwa miongoni mwa kampuni 40 zinazochipukia (Startups) za Afrika zilizoteuliwa kuingia katika awamu ya kwanza ya Programu ya Maandalizi ya Uwekezaji inayoendeshwa na kampuni ya Seedstars ya nchini Uswisi. 

Programu hiyo iliyopewa jina la ‘Investment Readiness Programme’ inalenga kuzijengea uwezo startaps za Afrika zinazotumia teknolojia kuwa na sifa za kupokea uwekezaji ili kuendeleza shughuli zao kwenye jamii. 

Katika hatua za awali za programu hiyo ya miezi mitatu iliyozinduliwa Mei mwaka huu, kampuni hizo zitakuwa na siku maalum za kuwasilisha mawazo ya kampuni katika maeneo yao ili kubaini maeneo yenye changamoto. 

Uwasilishaji wa mawazo hayo utafanyika katika miji minne ya Lagos, Cape Town, Cairo na Dar es Salaam.  Startups hizo 40 zilizochaguliwa zinajumuisha 17 za Misri, Nigeria (10), Afrika Kusini (10) na Tanzania (5). 

Kwa mujibu wa mtandao wa Ventureburn, startups hizo zilipatikana baada ya kupitia mchujo wa maombi 700 duniani kote katika awamu ya kwanza ambapo startups 78 zilichaguliwa zikiwemo 40 za Afrika. 

Programu hiyo inaendeshwa katika ofisi za Seedstars katika maeneo mbalimbali ya Afrika ambapo startups zilizochaguliwa zinajengewa uwezo na kupewa mafunzo juu ya uendeshaji kampuni wenye faida. 


Soma zaidi: Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google


Startups zote zinafuatiliwa na kufanyiwa tathmini ya kina wakati wote wa programu hiyo na kuangalia maeneo yenye changamoto kwa kila kampuni ili kuyapatia suluhu ili kujiweka tayari kwa ajili uwekezaji. 

Mafunzo hayo yanatolewa na wakufunzi wa ndani na nje ya Afrika kwa njia mbalimbali ikiwemo  video (teleconferencing). 

“Tuna mchanganyiko wa wataalam wa ndani na nje wenye uwezo mzuri wa mada zinazofundishwa, lakini tutaongeza maudhui kulingana na mahitaji,” amesema Ofisa Mwekezaji Mkuu wa  Seedstars, Charlie Graham-Brown wakati akihojiwa na Ventureburn. 

Masomo yanayofundishwa katika programu hiyo ni pamoja na teknolojia na uendeshaji, mapato na ukuaji, masula ya fedha na upimaji wa utendaji wa kampuni, sheria na utawala na jinsi ya kuvutia wawekezaji kwenye kampuni. 

Nukta Africa inamiliki tovuti ya habari ya nukta.co.tz na hufanya mafunzo kwa wanahabari na wadau wengine katika uandishi wa habari za takwimu na matumizi ya dijitali katika kuzalisha habari. 

Startups za Tanzania zilizochaguliwa ni KilimoGuide, FixChap, Peter’s Daughter, Kasome International na Nukta. Wakati kutoka Nigeria ni LUCY.NG, Resoltz, Bitmama, Ttysoon Cards Limited, MaiFarmland, Go Africa LLC, Farmz2U, Excrow, Joanswood Creation limited na One Kiosk Africa

Zilizofanikiwa kupenya kutoka Afrika Kusini ni Tellos, Kuba, LeadRobot, Work Wanderers, Ingede Group, Eazyloop Express, Boundless Aviation na Sxuirrel, huku Misri ikiingiza startups za Oddigo, Pashakim, Elmetr, Lira, The Mealkit, Vetwork, Furnwish, Reshrimp, ElMawkea, Guided, Koay, Hirebits, Forera, Mak, Hovo, Curotrip, na Egygarage. 

Enable Notifications OK No thanks