Anachokitaka Magufuli kutoka kwa Bashe, Simbachawene
- Awataka wakifanye kilimo kiwe na tija na kuharakisha utolewaji vibali vya mazingira vya Nemc kwa wawekezaji.
- Amewataka kutimiza majukumu yao kikamilifu kwa kushirikiana na wananchi.
- Bashe ameagizwa kutimiza kwa vitendo yale yote aliyokuwa anashauri akiwa Bungeni katika sekta ya kilimo.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka mawaziri wawili walioteuliwa jana, George Simbachawene na Hussein Bashe kutatua changamoto katika wizara zao ikiwemo kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa na tija na kuharakisha utoaji wa vibali vya mazingira vya ujenzi wa viwanda kwa wawekezaji.
Simbachawene ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa huku Bashe akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Julai 22, 2019) muda mfupi baada ya kuwaapisha mawaziri hao Ikulu jijini Dar es Salaam, amewapongeza kwa nafasi walizopata lakini amewataka wawe wavumilivu katika kuzikabili changamoto na kutimiza majukumu ya wizara zao.
“Kwa ujumla mimi nawapongeza, mkamtangulize Mungu, mtapigwa vita, mtazungumzwa mengine muyavumilie mumuachie Mungu kwa sababu Mungu ndiye ametaka nyinyi muwe katika nafasi zenu. Kashirikianeni na wanyonge ili mfanye makubwa,” amesema Rais.
Amesema ana matumaini makubwa kuwa mawaziri hao watatimiza majukumu yao na kuleta mabadiliko katika sekta za kilimo na mazingira.
Hata hivyo, Rais Magufuli amemtaka Naibu Waziri wa Kilimo, Bashe kutimiza kwa vitendo mambo yote aliyokuwa akishauri akiwa Bungeni kuhusu sera nzuri za kilimo zinavyoweza kuleta matokeo katika uzalishaji viwandani.
“Nimekuwa nakusikiliza sana Bungeni, michango yako imekuwa mizuri unatoa analysis (uchambuzi) ya namna kilimo kinavyoweza kuleta production (uzalishaji), kikaleta effect (matokeo) katika uchumi wa nchi yetu. Uchambuzi ule nimeupenda.
“Sasa zile zilikuwa za bungeni nataka sasa ukaziweke kwenye practical (matendo), ndiyo maana nimekuweka Wizara ya Kilimo, hayo yote uliyokuwa ukizungumza bungeni na tukafurahia sasa yakawe kwenye practical. Sasa ukayatende kweli kweli,” amesema Rais.
Amemtaka Naibu Waziri huyo kushughulikia changamoto za wakulima ikiwemo ya mazao ya kahawa na pamba ili kuhakikisha wanapata soko la uhakika.
Zinazohusiana:
- Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda
Akizungumzia kuhusu mazingira, Rais Magufuli amemtaka Simbachawene kushughulikia changamoto zake ikiwemo suala la Muungano na matumizi mabaya ya fedha za wafadhili zinazoelekezwa kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini.
“Katika masuala ya mazingira, wewe mwenyewe umeeleza hapa kuna fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa kule lakini impact (matokeo) yake haionekani. Kuna idara kule ya mazingira, fedha nyingi zinatolewa na wafadhili lakini haziwi reflected kwenye miradi husika,” amesema Rais.
Pia amemtaka Simbachawene kushughulikia changamoto ya uchelewashaji wa vibali vya mazingira vinavyotolewa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa wawekezaji ili kuharakisha ujenzi wa viwanda nchini.
“Vibali kwa mfano vya NEMC, pasiwe na uchelewaji wa vibali kwa wawekezaji kwa viwanda vyetu. Sisi tunataka tuwe na viwanda vya kutosha. Wawekezaji wasiwekewe vipingamizi kwa visingizio vya NEMC, vibali hivi vitoke kwa sababu tunahitaji viwanda,” amesema Rais.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene muda mfupi kabla ya kuapishwa Ikulu Jijini Dar es Salaam leo. Picha|Mtandao.
Kwa upande wake, Bashe akizungumza mara baada ya kuapishwa amesema nafasi aliyopewa katika Wizara ya Kilimo siyo kuitwa Mheshimiwa bali kusaidiana na watendaji katika wizara hiyo kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa na tija ikiwemo kukuza uchumi wa nchi.
“Mhe. Rais napenda nikuahidi wewe na mbele ya viongozi walio mbele yangu kwamba nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha kwamba natimiza yale yaliyo ndani ya mamlaka niliyopewa ili kuweza kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele,” amesema Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini.
Naye, Simbachawane amesema atashirikiana na wataalam katika wizara anayoiongoza ili kuhakikisha wanaokoa mazingira kwa kusimamia vizuri fedha za wafadhili zinazotolewa kutekeleza miradi ya kuzuia uharibifu wa mazingira.
Amesema kwa upande wa muungano atalisimamia lakini anahitaji kujifunza zaidi katika suala hilo.
“Na mimi kwa kushirikiana na wenzangu nitakaowakuta wakiwemo wataalam katika ofisi hii, nitajitahidi na mimi nitoe mawazo yangu ya namna gani tuweze kushughulikia ili kuokoa uharibifu mkubwa wa mazingira,” amesema Simbachawene.
Latest
