Majaliwa azindua Wiki ya Kagera, awapa mtihani wawekezaji
- Amesema uwekezaji unaofanyika katika mkoa huo uwanufaishe wananchi na kukuza pato la Taifa.
- Kagera inachangia asilimia 3.9 ya pato la Taifa.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema anataka kuona uwekezaji unaofanyika katika mkoa wa Kagera unawanufaisha wananchi na kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa hasa katika sekta za kilimo na viwanda.
Majaliwa aliyekua akizungumza leo (Agosti 14, 2019) wakati akizindua kongamano la Wiki ya Kagera na Mwongozo wa Uwekezaji lililofanyika Bukoba mjini amewataka wananchi wachangamkie fursa za biashara zilizopo mkoani humo.
“Ni ukweli usiofichika kwamba tunahitaji wawekezaji watakaosaidia uchumi wa mkoa huu kukua kwa kasi kupitia fursa zilizopo kwenye nyanja za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, maliasili na utalii,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ukuaji mzuri wa uchumi wa mkoa huo utakuwa na manufaa katika kuongezeka kwa pato la mwananchi wa Kagera, pato la mkoa na hata pato la Taifa nalo litakuwa kwa kasi ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Amesema mkoa wa Kagera ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa kahawa nchini, ambapo zaidi ya nusu ya kahawa yote huzalishwa katika mkoa huo.
“Wastani wa uzalishaji wa kahawa kwa mwaka ni kati ya tani 50,000 hadi tani 65,000 kutegemea na hali ya hewa ya mwaka husika,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Zinazohusiana:
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho.
- Wakulima wa korosho wameenza kulipwa-Majaliwa
Pia mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa michache Tanzania yenye fursa nyingi za uwekezaji ambazo kwa namna moja au nyingine hazipatikani katika mikoa mingine ya nchini.
Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na viwanda vya kukoboa na kusindika kahawa na soko la bidhaa kwani unapakana na nchi nne za Afrika Mashariki.
“Kagera imepakana na Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya. Kupakana na nchi hizo zenye idadi kubwa ya watu katika ukanda huu wanaokadiriwa kufikia takriban milioni 190 ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018 ni fursa ya uwepo wa soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa au zinazoweza kuzalishwa katika mkoa wa Kagera,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, baada ya kufungua kongamano la uwekezaji mkoani Kagera, Agosti 14.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafiri ukiwemo wa anga na wa barabara ili kurahisisha usafiri kutoka Bukoba makao makuu ya mkoa wa Kagera kufika katika nchi hizo.
“Kwa mfano, umbali kutoka Bukoba hadi Kampala ni kilomita 340, Bujumbura (kilomita 550) na Kigali (kilomita 490). Kadhalika, itakuwa ni rahisi kufikia masoko ya nchi za Sudan Kusini pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC),” amesema Waziri Mkuu.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema dhamira ya kuandaliwa kwa wiki ya uwekezaji mkoani Kagera ina lengo la kuhakikisha kwamba mkoa huo unafanya vizuri katika sekta ya uwezekezaji na biashara, hivyo kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa.
Amesema mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo ina mchango mdogo katika pato la Taifa, hivyo wanataka watoke kwenye kuchangia asilimia 3.9 hadi wafikie asilimia 10.