Pigo jingine kwa Rayvanny: Serikali ya Kenya yafungia wimbo wa Tetema

August 27, 2019 2:26 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Huu ni wimbo wa pili wa Rayvanny kufungiwa kwa sababu ya maadili ndani ya miezi tisa.
  • Basata yasema lugha na mapokezi ya nyimbo hiyo inatofautiana baina ya nchi na nchi.
  • WCB wasema hawana taarifa rasmi na hawaoni tatizo katika wimbo huo.

Dar es Salaam. Wiki tatu baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya Rayvanny atoe remix ya wimbo wake wa “Tetema” akiwashirikisha wasanii wa kimataifa akiwemo Pitbull wa Marekani, msanii huyo amejikuta akiingia kwenye hasara nyingine baada ya Serikali ya Kenya kuufungia wimbo huo kwa madai kuwa umejaa “maudhui ya ngono”.

Kufungiwa kwa wimbo huo wa Tetema nchini Kenya kunafanya Rayvanny kupoteza fursa za kimapato katika nyimbo mbili kwa kipindi cha miezi nane ikiwa wimbo wake wa “Mwanza” ambao pia amemshirikisha Platnumz ulifungwa 12 Novemba 2018 ikiwa na sababu zilezile za kukosa maadili.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KFCB, Ezekiel Mtua amewaambia wanahabari nchini Kenya leo (Agosti 27,2019) kuwa maneno ya wimbo huo “ni machafu na hayafai kusikilizwa na umma hasa mazingira ambayo watoto wanaweza kusikiliza ama kutizama.”

Sanjari na Tetema mamlaka hiyo imeufungia wimbo mwingine nchini humo unaopendwa zaidi na vijana uitwao Wamlambez.

Mutua amesema nyimbo hizo mbili haziruhusiwi kuchezwa nje ya klabu za usiku na vilabu vya pombe maarufu kama baa.

“Nyimbo hizo zina maudhi yote ya ngono. Japo kuwa hatutaweza kuzifuta kabisa kwa sababu lugha imefichwa lakini ni vema umma ukafahamu kuwa ni chafu na hazifai kupigwa katika mazingira ya familia. Tuziache zipigwe katika vilabu vya pombe kwa ajili ya wakubwa pekee,” ameongeza Mutua katika ukurasa wake wa Twitter.

Uamuzi wa Bodi ya Filamu ya Kenya (KFCB) kuufungia wimbo huo, ni mwendelezo wa maumivu kwa msanii huyo na lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) baada ya mamlaka nchini Tanzania kuufungia pia wimbo mwingine wa Mwanza maarufu Nyegezi miezi tisa iliyopita. Wimbo huo wa Mwanza, aliokuwa amemshirikisha bosi wake Diamond Platnumz ulipigwa marufuku ndani na nje ya nchi na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Novemba 2018 kwa sababu zile zile za “kukosa maadili”.

Wakati Kenya wakiuzuia Tetema kupigwa katika maeneo ya umma yenye watu mchanganyiko wakiwemo watoto, tayari wimbo huo ulikuwa sokoni tangu tangu Februari 7, 2019. 

Hadi leo saa 11 jioni Agosti 27, 2019  video ya wimbo huo iliyopo katika mtandao wa Youtube ilikuwa na watazamaji milioni 27.18 huku Remix yake aliyemshirikisha Diamond Platnumz, Muhombi, Joen na Pitbull ambayo ni sauti pekee ikiwa na watizamaji 475,477.

Kuzuiawa kwa wimbo huo katika matamasha ya wazi nchini Kenya ni pigo jingine kwa msanii huyo kimapato kwa kuwa ni moja ya nyimbo ambazo zimempatia mafanikio kimuziki na kujulikana kimataifa. Ni Tetema pekee iliyoweza kupata watizamaji zaidi ya milioni 20 Youtube ikifuatiwa na wimbo wa Kwetu uliotolewa miaka mitatu iliyopita wenye watazamaji milioni 19.2.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, wimbo huo unaendelea kupigwa Tanzania huku Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza akieleza kuwa “haoni ubaya wowote” kwenye wimbo huo.

Mngereza ameiambia Nukta Habari kuwa Basata haina taarifa za kufungiwa wimbo huo Kenya na kwamba Tanzania na Kenya ni nchi mbili tofauti zenye sheria na taratibu zake zinatofautiana.

Bosi huyo wa Basata amesema jambao ambalo linachukuliwa kuwa tofauti na maadili nchini Kenya haliwezi fanana na Tanzania.

“Kuna baadhi ya maneno ya kijapani ambayo kwa lugha ya kiswahili ni maneno mazito hivyo huenda hali ikawa sawa na hivyo nchini kenya,” amesema Mngereza na kuongeza kila msanii anapotoa wimbo anakuwa amelenga makundi tofauti tofauti kwenye jamii hivyo sio kila wimbo unamfaa kila mtu.

Amesema zipo baadhi ya nyimbo ambazo zinafaa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 na zina maeneo maalumu ya kusikilizwa kama baa na labu za usiku ambapo watu wenye rika hilo hukusanyika.

Tetema ni wimbo uliompa mafanikio zaidi Rayvanny kwani umetizamwa zaidi ya mara milioni 20. Picha|WCB

Licha ya wimbo huo kuzuiwa Kenya, uongozi wa WCB ambao unamsimamia Rayvanny umeeleza kuwa hauna taarifa rasmi kutoka Kenya na kwamba hauoni tatizo lolote kwenye wimbo huo.

Meneja wa wasanii wa WCB, Hamisi Taletale ameiambia Nukta kuwa  ambaye amekiri kuziona taarifa hizo kwenye mtandao na kusema kuwa hawaoni tatizo katika wimbo huo.

“Uamuzi wao haushushi uchumi wa kampuni bali unapandisha kwani wimbo ukizuiwa, watu wanashtuka wanaanza kuufatilia kwenye mtandao wa Youtube,” amesema Babu Tale bila kueleza kwa kina kuhusu mapato yanayohusu wimbo huo.

“Hakuna cha kufanyika kwani ni muhimu kuheshimu mamlaka. Ikiwa Basata wameupitisha wao wana yao,” amesema Babu Tale.

Kwa bahati mbaya, nyimbo zote ambazo Rayvanny zimeingia kwenye mgogoro na mamlaka ni zile ambazo amemshirikisha Diamond Platnumz.

Enable Notifications OK No thanks