Sababu za ndege ya Air Tanzania kuachiwa Afrika Kusini
Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema mahakama ya Gauteng ya nchini Afrika Kusini leo Septemba 4, 2019 imeamuru ndege ya Air Tanzania (ATCL) Airbus A220-300 iliyokuwa inashikiliwa nchini humo kuachiwa.
Mahakama Kuu ya Gauteng, Afrika Kusini, leo imetoa hukumu na kuamuru kuwa ndege ya @AirTanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi. Tunawashukuru wote kwa uvumilivu wenu.
Dkt. H.A.
— Msemaji Mkuu wa Serikali (@TZMsemajiMkuu) September 4, 2019
Mahakama hiyo imeamtaka raia wa Afrika Kusini, Hermanus Steyn aliyefungua kesi akitaka kulipwa Dola za Marekani milioni 33 kulipa gharama za kesi hiyo baada ya kushindwa.
“…Hoja zote zilizotolewa na mawakili wetu zimeshinda, na tumeshinda kesi hiyo, na imeamriwa ndege hiyo #AirTanzania iweze kuondoka,” Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Dk Damas Ndumbaro.
Ndege hiyo ilizuiliwa tangu Agosti 23, 2019 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wa Johannesburg imezuiliwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg, jambo lililoibua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii.
Akitoa taarifa rasmi ya Serikali, leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ni kweli ndege hiyo imeachia rasmi na itaendelea na shughuli zake za kawaida.
“Ndege yetu Airbus ya ATCL ambayo ilikuwa imeizuiliwa Afrika Kusini ikiwa katika shughuli zake leo imeachiwa rasmi. Inarudi katika aratiba zake za kawaida,” amesema Waziri huyo.
Amebainisha kuwa Watanzania wanaipenda ndege yao na sasa itarudi huku akiweka wazi kuwa Serikali iko mbioni kununua ndege nyingine.
“Nashukuru nilikuwa na tenson kubwa, Watanzania wanapenda kupanda ndege ya kwao ya ATCL. Kwa hiyo ratiba ile iliyokuwa inayumba yumba ndugu zangu Watanzania sasa inarudi. Tunaendelea na ununuzi wa ndege nyingine mbili. Tupo vizuri,” amesema.