Rejesha ardhi katika ubora wake ili kukuza uchumi:Thiaw
Thiaw alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kwa njia ya video kutoka New Delhi, India ambako anashiriki mkutano wa mkataba huo (COP14), unaofanyika tangu Septemba 2 hadi 13 ukiwa na kaulimbiu “kuwekeza katika ardhi, kufungua fursa”. Picha|Mtandao.
- Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Jangwa (UNCCD), Ibrahim Thiaw amesema dunia sasa inatakiwa kuwekeza katika urejeshaji wa ardhi katika ubora wake.
- Itasaidia kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazoweza kuyumbisha uchumi.
Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Jangwa (UNCCD), Ibrahim Thiaw amesema dunia sasa inatakiwa kuwekeza katika urejeshaji wa ardhi katika ubora kama njia mojawapo ya kuboresha ustawi wa maisha, kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazoweza kuyumbisha uchumi.
Thiaw alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani kwa njia ya video kutoka New Delhi, India ambako anashiriki mkutano wa mkataba huo (COP14), unaofanyika tangu Septemba 2 hadi 13 ukiwa na kaulimbiu “kuwekeza katika ardhi, kufungua fursa”.
“Ardhi inatupatia asilimia 99.7 ya nguvu tunazopata na maji tunayokunywa. Ardhi ni mchangiaji mkubwa katika uchumi wetu. Pia ina uhusiano na afya yetu. Dhoruba za mchanga na vumbi ni visababishi vya matatizo katika maeneo mengi ya dunia hususani yanayohusiana na magonjwa kama pumu,” amesema Thiaw.
Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN), Thiaw amesema katika mwaka uliopita yaaani 2018, nchi 25 ziliingia katika dharura ya ukame; Zaidi ya nchi 70 zimeathirika na ukame na nchi za namna hiyo zinahangaika na uhaba wa chakula.
Zinazohusiana:
- PASS kuwawezesha vijana sekta ya kilimobiashara.
- Kigoma kinara usajili mashamba Tanzania bara.
- Uongozi, ardhi kuwatoa kimaisha wanawake vijijini.
Aidha, ameeleza kuwa kuna uhusiano kati ya amani na usalama, “hali katika eneo la Sahel (jangwa la Sahara) ni mchanganyiko wa sababu nyingi zikiwemo kushindania ardhi na maji. Watu wengi walioathirika wako barani Asia na eneo lililoathirika zaidi ni Afrika.”
Akijibu maswali ya Wanahabari, Thiaw amesema mkutano unaoendelea India unategemewa kukubaliana kuhusu maamuzi 30 katika mpango wa kuhakikisha malengo ya mwaka 2018 hadi 2030 yanafikiwa.
Pande zote zinazoshiriki zitapitisha makubaliano kuhusu udhibiti wa mmomonyoko wa udongo ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa UN wa mabadiliko ya tabianchi mnamo Septemba 23 mwaka huu ambao utaeleza kuwa uboreshaji wa ardhi ni sehemu moja ya suluhisho katika kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.