Petroli, mafuta ya taa vyachangia kushusha mfumuko wa bei
- Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma umeshuka hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019 kutoka asilimia 3.7 iliyorekodiwa Julai mwaka huu.
- Kushuka huko kumechangia zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za chakula ikiwemo petroli na mafuta ya taa.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania umeshuka hadi kufikia asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019 kutoka asilimia 3.7 iliyorekodiwa Julai mwaka huu, ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za chakula.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Sepetemba 9, 2019), imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa hasa zisizokuwa za chakula ikilinganishwa na Julai mwaka huu.
Mfumko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula ambazo umeshuka ni pamoja na mafuta ya taa ambayo yamepungua kwa asilimia 2.6, petroli kwa asilimia 4.3 na majiko ya gesi kwa asilimia 1.4,
Pia gharama za kufanya ukarabati wa nyumba (1.7) na bidhaa za usafi binafsi ikiwemo mafuta ya nywele (1.3).
Zinazohusiana: Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Januari
Kwa upande wa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeongezeka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 2.9 kama ilivyorekodiwa Julai 2019.
Sambamba na bidhaa hizo, bidhaa na huduma zingine kama hoteli, migahawa na huduma za elimu hazijabadilika kabisa huku huduma za tamaduni na mapumziko (recreation) zikishuka kwa asilimia 0.4.
“Kushuka kwa mfumuko wa bei kunaelezea kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka zimeishia ulioishia mwezi Agosti 2019.” inasomeka sehemu ya ripoti ya mfumuko wa bei ya NBS iliyotolewa Jumatatu (Septemba 9, 2019)
NBS imesema kasi ya mabadiliko ya bei ya Agosti 2019 ipo chini ikilinganishwa ni ile iliyorekodiwa Julai 2019.