Shule ya Sekondari Patmos: Kilele cha mafanikio kilichojificha Kilimanjaro
- Ndani ya miaka sita tangu kuanzishwa kwake, Patmos imekua kwa kasi kitaaluma kiasi cha kuzibwaga shule kongwe.
- Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule hiyo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20, kiwango ambacho ni bora mara mbili ya kile kinachopendekezwa na Serikali.
- Shule hiyo ni kimbilio la wazazi na walezi wenye watoto watukutu kwa kuwa hufundisha nidhamu na kuwarejesha katika tabia inayotakiwa katika jamii.
Moshi. Kilomita saba, ndani kidogo, kutoka katika barabara ya Arusha-Moshi, inapatikana Shule ya Sekondari ya Patmos ambayo ni moja ya shule chache nchini zilizojikita kumwezesha mwanafunzi kupata elimu bora na maarifa ya kuishi na jamii.
Shule hiyo, iliyopo wilayani Hai katika mkoa wa Kilimanjaro, mbali na kutoa elimu bora kwa watoto wote, imekuwa ni kimbilio la wazazi wenye watoto wakorofi kutokana na uwezo mkubwa wa walimu kuwabadilisha tabia wanafunzi hao.
Ndani ya miaka sita tangu kuanzishwa kwake, Patmos imekua kwa kasi kitaaluma kiasi cha kuzibwaga shule kongwe katika mkoa wa Kilimanjaro wenye shule nyingi zaidi za sekondari nchini.
Mkuu wa Taaluma wa shule hiyo Mwalimu, Josephat Ulomi amesema moja kati ya mafanikio ya shule hiyo ni pamoja na kusimamia nidhamu huku usimamizi huo ukifanikiwa kuondoa sifuri katika shule hiyo. Sifuri ni moja ya mwiba mkali unaozitesa shule nyingi za umma na binafsi Tanzania.
“Sera ya shule yetu ni hamasa, mafunzo na nidhamu. Tunafundisha wanafunzi wetu kuwa na hofu ya Mungu na kuhakikisha kati yao hakuna anayeachwa nyuma,” amesema Mwalimu Ulomi.

Mbali na kufundishwa vema masomo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Patmos hufundishwa maadili mema na ujasiriamali ili kuwaandaa vema vijana na mahitaji ya soko. Picha|Patmos.
Mwalimu huyo pia alisisitiza kuwa yote hayo yamefanikiwa kwa kuwepo miundombinu mizuri ya shule ikiwa ni pamoja na hosteli kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume ambapo gharama ya hosteli hizo inajumuishwa kwenye ada.
Kawaida kwa mwanafunzi ada inayojumuisha na gharama za hosteli, kitambulisho, godoro na safari ya Nane Nane kila mwaka ni Shilingi milioni1,650,000 huku wale wasiohitaji huduma za hosteli wakilipia Shilingi 900,000 tu.
Hata hivyo, Mwalimu Ulomi amesema asilimia 98 ya wanafunzi wote wanalipia hosteli hivyo kufanya maendeleo yao kitaaluma kuwa mazuri kwa kuwa wasimamizi wa wanafunzi wa hosteli wanaishi kwenye makazi yao kwenye mazingira hayo hayo.
Patmos iliyoanza kutambulika rasmi na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), miaka mitano iliyopita, ina jumla ya walimu 11 huku ikiwa na wanafunzi 200. Idadi hiyo ya walimu inafanya Patmos kuwa ni moja ya shule nchini zenye uwiano mzuri zaidi wa mwalimu kwa wanafunzi.
Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule hiyo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20, kiwango ambacho ni bora mara mbili ya kile kinachopendekezwa na Serikali cha mwalimu mmoja wanafunzi 40 hadi 45.
Pamoja na kuwa tayari ina uwiano mzuri wa wanafunzi, menejimenti ya shule hiyo imeeleza kuwa kwenye mchakato wa kuongeza mwalimu mbobezi wa somo la Kiswahili ili kuhakikisha wanafunzi wanapigwa msasa kikamilifu katika lugha hiyo ya Taifa.
Kwa kipindi hicho chote, takwimu za NECTA zinabainisha kuwa shule hiyo imekuwa na ufaulu mzuri huku matokeo yake yakiwa ni mwendo wa madaraja ya kwanza, pili, na tatu huku wachache wakipata daraja la nne. Ndani ya miaka mitano iliyopita Patmos haijawahi kupata daraja sifuri.
Matokeo hayo yameiwezesha shule hiyo kuwa shule ya tano kimkoa mwaka 2015 na ya 8 kimkoa mwaka 2016 kwa shule zenye wanafunzi chini ya 45 huku ikiwa kiboko ya masomo ya Kiingereza, Hesabu na Jiografia.

Faida lukuki nje ya masomo
Mwalimu Ulomi amesema wanafunzi wa shule hiyo hufaidika na mikutano mbalimbali inayo wakutanisha na wabobezi wa taaluma mbalimbali ambao huwapa motisha ya kufikia ndoto zao na kuwasisitiza juu ya vipaumbele wanavyotakiwa kuvizingatia ili kufikia safari hiyo.
“Tunawakutanisha wanafunzi na madaktari na hata mainjinia ambao huwapa motisha ya safari ya ndoto zao pia safari za kitalii huwawezesha kuona uzuri wa nchi yetu…tumeshawapeleka Zanzibar, Ngorongoro na sehemu zingine nyingi tu,” amesema Mwalimu Ulomi.
Sambamba na taaluma kuwa kipaumbele cha shule hiyo, Patmos haijaacha kutoa fursa za ajira kwani kwa sasa inatafuta mtaalamu wa miradi ya ufugaji.
Elimu ya ujasiriamali kwa sasa imekuwa ikisisitizwa ili kuwasaidia vijana kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao badala ya kusubiri ajira ambazo zimezidi kuwa adimu siku hadi siku.
Licha ya kuwa wameshaanza kupanda ngazi kwa kasi, malengo makubwa ya shule hiyo ni kuendelea kutoa elimu bora ya taaluma na kujitegemea na kufikia hatua ya kuwa namba moja nchini.

Makala haya ya mtangazaji yametolewa na Shule ya Sekondari ya Patmos iliyopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Kwa maoni au maulizo wasiliana nasi kupitia baruapepe: client@nukta.co.tz.