Majaliwa awakomalia viongozi Morogoro, amsimamisha kazi mtendaji mwingine

September 18, 2019 2:08 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Injinia, Godfrey Mlowe (kulia), baada ya kukagua jengo la kituo cha afya Mkuyuni, kilichopo katika Wilaya ya Morogoro, Septemba 18.2019. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Ni Mhandisi wa ujenzi wa wilaya ya Morogoro, Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
  • Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti.
  • Amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe kuchunguza vizuri mkoa wake kwa sababu umekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa ujenzi wa wilaya ya Morogoro, Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha afya Mkuyuni.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mussa Mnyeti.

Kutenguliwa kwa viongozi hao ni kutokana na kutokuwepo kwa maelewano kati yao na kusababisha kusua sua kwa shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo. 

Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi huyo leo (Septemba 18, 2019) baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Mkuyuni akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro. 

Maamuzi hayo yamekuja baada ya kutokuridhishwa na aina ya milango iliyotumika katika kituo hicho. 

“Milango yote katika jengo hili ing’olewe leo leo, huwezi kuweka milango ya hovyo namna hii yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha kuendelea kukagua jengo. Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya hovyo kama hii,” amesema Majaliwa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na uangalizi mbovu kutoka kwa watendaji walikubali kuweka milango hiyo mibovu.


Soma zaidi: 


Amesema Serikali imeamua kujenga vituo vya afya vitano kwenye wilaya hiyo ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, hivyo amewataka watendaji wasimamie ipasavyo miradi hiyo.

Baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambako nako ameagiza kuong’olewa kwa mbao zote zilizotumika kwa ajili ya kupaulia jengo la mama na mtoto la hospitali hiyo kwa kuwa hazina viwango. 

“Fundi usiendelee na kazi hii ya upauaji kwa sababu mbao unazotumia hazikidhi viwango,” amesema Majaliwa.

Fundi anayejenga jengo hilo la mama na mtoto, Johnson Ishengoma amesema changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa vifaa pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.

“Mhandisi wa wilaya, Brown Undule na mtu wa manunuzi Grace ndio wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa navikataa kutokana na kutokuwa na ubora,” amesema Ishengoma.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe kuuangalia vizuri na kuhakikisha anauchunga vizuri mkoa wake kwa sababu umekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Enable Notifications OK No thanks