Petroli, majiko ya gesi vyachangia kushusha mfumuko wa bei
- Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019 umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.
- Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji umepanda hadi asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini umeshuka hadi kufikia asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019 kutoka asilimia 3.6 iliyorekodiwa Agosti mwaka huu, ikichagizwa zaidi na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula ikiwemo mafuta ya taa na petroli.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo, kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo mafuta ya taa, petroli na majiko ya gesi.
“Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2019 umepungua hadi asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2019.” inasomeka taarifa ya NBS.
Mfumko wa bei ya mafuta ya taa umepungua kwa asilimia moja huku petroli ikipungua kwa asilimia 3.3 na majiko ya gesi yakishuka kwa asilimia 1.5.
Bidhaa nyingine ni dawa za kuulia wadudu nyumbani ambayo imeshuka kwa asilimia 2.2 na mafuta ya nywele kwa asilimia 1.3.
Zinazohusiana
Kushuka kwa kasi ya mfumuko bei kunamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Septemba 2019 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Agosti 2019.
Aidha, kushuka kwa mfumuko wa bei hasa katika bidhaa na huduma zisizo za vyakula ni mwendelezo wa kushuka kwa mfumuko huo kwani tangu mwaka ulioishia Julai 2019, umekuwa ukishuka mfululizo kwa viwango tofauti.
Hata hivyo, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji umepanda hadi asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia Agosti 2019.