Magufuli: Anzisheni bustani za wanyamapori kukuza ajira, utalii
- Amesema itasaidia kuongeza idadi ya wanyama hao na hivyo kupanua fursa za utalii na ajira.
- Amewataka wataalam wa wanyamapori kuwafundisha wananchi kufuga wanyama hao.
- Kwa sasa Tanzania ina Zoo 23, Mashamba ya wanyama 20 na ranchi sita.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wengi zaidi kujitokeza kufuga wanyamapori katika bustani za wanyama (Zoo) ili kuongeza idadi ya wanyama hao na hivyo kupanua fursa za utalii na ajira.
Amewapongeza baadhi ya Watanzania walioanzisha Zoo hizo wakiwemo Luteni Jenerali Mstaafu, Samwel Ndomba ambaye anamiliki Lugari Mini Zoo iliyopo Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Dar es Salaam Zoo, Bahari Zoo na wengine ambao wamefuga wanyamapori katika bustani na mashamba yao.
Amefafanua kuwa ufugaji wa wanyamapori unaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kwamba Watanzania wanayo haki ya kuwapata wanyamapori hao na kuwafuga mahali popote panapofaa na patakapowezesha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea.
“Kuna nchi nyingi ambazo wenzetu wananufaika sana kwa ufugaji huu wa wanyamapori ikiwemo Afrika Kusini, wanapata watalii wengi, watu wao wanapata ajira na wanaowekeza kwenye ufugaji huu wanapata fedha, sioni sababu kwa nini sisi Watanzania tusifuge wanyamapori wakati sheria zinaruhusu kufanya hivyo.
“Changamkieni fursa hii ndugu zangu, wataalamu wa wanyamapori wafundisheni wananchi kufuga wanyamapori na wahamasisheni kufanya hivyo, viongozi wastaafu jitokezeni kuonesha mfano kama alivyofanya Lut. Jen. Mstaafu Ndomba kule Mbinga, maeneo ya kufuga yapo mengi,” amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Maafisa na Askari Wanyamapori wa Hifadhi za Taifa (Tanapa) waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
Zinazohusiana:
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
- Serikali yajipanga kuwapandikiza Sokwemtu katika hifadhi za Ibanda na Rumanyika
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kupanua na kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii ambapo katika miaka minne iliyopita hifadhi za Taifa zimeongezwa kutoka 16 hadi 22 na nyingine zikiwa mbioni kuanzishwa, kutokana na kutambua kuwa utalii ni sekta inayochangia vizuri katika pato la Taifa na inayotoa ajira kwa Watanzania wengi.
Kwa sasa Tanzania ina Zoo 23, Mashamba ya wanyama 20 na ranchi sita.
Simba ni miongoni mwa wanyamapori wanaofugwa katika bustani ya Dar es Salaam Zoo. Picha|Mtandao
Taratibu za kufuga wanyamapori
Ufugaji wa wanyamapori ni kitendo cha kuhifadhi au kutunza wanyamapori nje ya mazingira yao ya asili huku wakihudumiwa na kupewa mahitaji yao muhimu.
Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007 na Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori ya mwaka 2009 na kanuni zake zinaeleza kuwa kabla ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa wanyamapori katika mashamba, bustani na ranchi za wanyamapori mwombaji anapaswa kuwa na eneo la mradi, kuandaa andiko la mradi na kupata ushauri wa wataalamu kuhusu mradi unaopendekezwa.
Pia anatakiwa kusajili mradi kwa Wakala wa Usajili na Leseni (Brela) jina la biashara au kampuni, kuhakikisha eneo la mradi lina endana na mpango wa atumizi ya ardhi na kufanya tathimini ya athari ya mazingira kwa mradi pendekezwa, kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Baada ya kusajili mradi wa ufugaji, mwombaji atatakiwa kuomba wanyamapori wa mbegu (parent stok) kwa ajili ya uendelezaji wa mradi .Wanyamapori hao wanaweza kukamatwa kutoka kwenye maeneo ya wazi au kutoka katika mashamba, bustani na ranchi za wanyamapori.
Sheria imetoa fursa ya kuingiza wanyamapori nchini kwa kuomba kibali cha kuingiza wanyamapori (Import permit).