Ufalme wa Diamond Platnumz, Harmonize watikiswa YouTube
- Leo (Januari 7, 2019) zimeibuka sura za wasanii wengine kwenye chati za ubora za Youtube ambazo awali zilishikiliwa na Diamond na Harmonise.
- Waliopanda nafasi za juu kabisa ni pamoja na Aslay na Ommy Dimpoz, Christian Bellla na Darassa.
- Diamond Platnumz bado anatetea taji lake kwenye kipengele cha Msanii bora.
Dar es Salaam. Imezoeleka kuwaona Diamond, Harmonize, Innos B na Alikiba wakizishikilia chati za ubora wa muziki za Youtube na kuwafanya kuwa wafalme katika mtandao huo.
Leo (Januari 7, 2019) zimeibuka sura za wasanii wengine kwenye chati hizo ambao hapo awali walishikilia nafasi za chini.
Kulingana na mpangilio wa wasanii, nyimbo na video bora za muziki kwa upande wa Tanzania katika mtandao huo, hawa ndiyo wageni waliofanikiwa kuingia 10 bora ya chati hizo siku ya leo:
Muziki unaovuma na kufuatiliwa zaidi ni Kata wake Ommy Dimpoz
Kwa muda mrefu, nafasi hii imekuwa ikishikiliwa na msanii Diamond Platnumz na mara kadhaa Harmonize na Rayvanny au Alikiba.
Licha ya ushindani huo, hadi kufikia mchana wa leo, msanii Ommy Dimpoz ameshikilia nafasi ya kwanza ya orodha hii baada ya wimbo wake wa “Kata” alioimba na Nandy kumuweka kwenye nafasi ya kwanza.
Nyuma yake, Dimpoz amefuatiwa na Harmonize katika nafasi ya pili aliyeingia na wimbo wa “Hainistui” kisha Mboso aliyeiona nafasi ya tatu kupitia wimbo wake wa “Ate”.
Zinazohusiana
- Innoss’B awapiga kikumbo wasanii wa Bongo Fleva Tanzania
- Maumivu, kicheko kwa wasanii mabadiliko chati za muziki Youtube
Video bora ni ya Mateka ya Aslay
Huenda ulitegemea kuona “Baba Lao” au hata “Uno” lakini Aslay kupitia video yake ya “Mateka” ndiye anayekalia kiti hiki cha enzi cha video bora katika nafasi ya kwanza.
Mateka ambayo imeonyesha simulizi ya aina yake, inafuatiwa na video ya wimbo wa “Yope” ya msanii Innos B na kisha “Baba Lao” yake Diamond Platnumz.
Msanii Bora ni Diamond Platnumz
Ndiyo. Kwa sasa ni Diamond Platnumz ambaye hivi karibuni, ametoa wimbo wake wa “Sound” akiwa na msanii wa Nigeria, Teni hadi kufikia leo mchana alikuwa na wafuasi zaidi ya milioni 2.8 walimfuatilia katika mtandao huo.
Msanii huyo ambaye anajulikana kama “Dangote” anashikilia nafasi hii baada ya nyimbo zake kuchezwa hadi kufikia watazamaji milioni 21.1.
Dangote anafuatiwa na Aslay na kisha kufuatiwa na Harmonize ambaye mshale wake wa umaarufu kwenye chati hiyo unashuka.
Mbali na sura hizo ngeni kwenye chati hizi, sura ya Darassa na Chistian Bella pia zimeonekana na unaweza kujua zitakaa kwa muda gani endapo utabaki na Nukta (www.nukta.co.tz)
Latest